Leila Sheikh alikuwa mwanahabari, mwanaharakati wa haki za wanawake na watoto, na mmoja wa wanawake muhimu katika historia ya harakati za kijinsia nchini Tanzania.
Alikuwa miongoni mwa waanzilishi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) kilichoanzishwa mwaka 1987. Kupitia TAMWA, Leila aliamini katika kutumia nguvu ya habari na uandishi wa habari kuibua masuala ambayo mara nyingi yalipuuzwa na jamii, hasa ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Leila pia aliwahi kuwa mhariri wa jarida la Sauti ya Siti, mojawapo ya majukwaa muhimu ya sauti za wanawake nchini Tanzania. Kupitia uandishi na uhariri wake, alisaidia kuleta mijadala kuhusu ukatili wa kijinsia, unyanyasaji wa kijinsia na haki za wanawake katika uwanja wa umma. Mwaka 1992, alisimamia toleo maalumu la Sauti ya Siti lililojikita katika ukatili dhidi ya wanawake.
Mwaka 1996, Leila akawa Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, nafasi aliyotumia kuendeleza kazi ya advocacy na kuimarisha sauti ya wanawake kupitia vyombo vya habari. Alishiriki pia katika mchakato wa advocacy uliosaidia kufanikisha kupitishwa kwa Sheria ya Makosa ya Kujamiiana ya mwaka 1998 (SOSPA), iliyokuwa hatua muhimu katika kuimarisha ulinzi wa wanawake na watoto dhidi ya ukatili wa kijinsia.
Mbali na kazi yake ndani ya TAMWA, Leila aliendelea kufanya kazi kama mshauri wa advocacy, mtayarishaji wa maudhui na mwandishi wa scripts. Alianzisha pia Studio Calabash, iliyojikita katika mikakati ya lobbying, advocacy na elimu kwa umma.
Leila Sheikh alifariki mwaka 2023, lakini urithi wake unaendelea kuonekana katika historia ya uandishi wa habari za kijinsia Tanzania. Alionyesha kwamba kalamu, habari na vyombo vya habari vinaweza kuwa nyenzo za kupinga ukosefu wa haki na kuleta mabadiliko katika jamii.