Mtaa wa Hekaheka
Naomi alipoingia kwenye mgahawa ule uliokuwa na wateja wengi, alisimama kwa dakika kadhaa huku akipepesa macho yake huku na kule. Kijana aliyekuwa anafurahia chakula chake kwa uma na kisu alipigwa na butwaa, akaacha kula. Alimkodolea macho Naomi kama mjusi aliyebanwa na mlango. Hatimaye Naomi alimwona mhudumu aliyevaa sketi fupi ya kitenge na shati jeupe lenye nembo ya mgahawa kifuani kwake akimsogelea na kumkaribisha katika meza iliyokuwa tupu. Naomi alisogea kwenye ile meza akaketi. Pembeni yake aliona meza iliyokuwa na sahani nne pana na kila sahani ilikuwa na kisu na uma wa shaba yae kung’aa. Tumbo lake lilinguruma mfano wa simba, lakini angeagiza nini na mfukoni alikuwa hana kitu?
“Nahitaji kumuona Bwana Kilonzo!” Naomi alisema baada ya ukimya wa muda mfupi. Mhudumu alimtazama kutoka juu mpaka chini na kubetua midomo yake kama aliyetaka kutema mate kwa kinyaa.
“Wewe ndo wa kumwona Mkurugenzi?”
“Ndio. Ananifahamu. We mwambie tu ni Naomi, mtoto wa Mama Naomi.” Naomi alimeza funda kidogo la mate na kumtazama muhudumu.
“Meneja….!” Mhudumu aliita kwa sauti kubwa iliyowafanya wateja wageukie upande ule.
“Eti huyu Msichana anataka kumwona Mkurugenzi!”
Kijana wa makamo aliyevalia suruali nyeusi na shati la kitenge kama kile cha sketi ya mhudumu, aliachia kitasa cha mlango na kugeuka kuwatazama Naomi na mhudumu. Nyuma mlango ulifunguka akatoka mzee mwenye mvi kichwani aliyevaa koti ambalo vishikizo havikufungamana barabara sababu ya kitambi chake na kuacha shati jeupe la hariri kuonekana.
Naomi alipiga hatua kumfuata yule mzee na macho yote ya wateja yakisafiri pamoja naye. Mzee Kilonzo alipunga mkono na alipokwisha shusha kila mhudumu alirudi kwenye kazi yake. Alimpisha Naomi apite, kisha naye aliurudishia mlango na kwa hatua za kuhesabu akaelekea kwenye kiti chake cheusi, akaketi na kujizungusha kulia na kushoto kumtazama Naomi.
“Najua una matatizo gani.” sauti ya mngurumo wa chini ilijaa ndani ya ofisi ile.
“Mmeishiwa chakula nyumbani?” Naomi alisimama katulia tuli kama sanamu akisubiri neno la pili kutoka kwa Mzee Kilonzo.
“Umekuja mwenyewe au mama yako amekutuma?”
“Nimekuja mwenyewe.” Kilonzo aliinuka taratibu na kumsogelea, akaagemeza mikono yake mizito katika mabega mawili ya Naomi.
“Nitakusaidia chochote unachotaka ukinisaidia chochote ninachotaka.”
Naomi alishusha uso na macho yake yakutua katika viati vyenye mng’alizo alivyovaa Mzee Kilonzo, yakapanda kutazama suruali ilivyoonyoshwa barabara na kuishia katika vidole vilivyosheheni pete za fedha na dhahabu.
Kauli yake ilitosha kumaliza shida zake zote. Angeweza kupata pesa ya kula, pango na mapambo ya mwili. Ghafla aliukumbuka uso wa mama yake uliokuwa umejaa simanzi waliopoagana asubuhi. Pengine mama yake angefurahi kwa chochote ambacho angeweza kumpelekea.
“Hii itakuwa siri yetu.” Kilonzo alinong’ona masikini mwa Naomi. Mama yako asijue.”
Naomi alifumba macho akavuta Taswira na kuzikumbuka siku zile Kilonzo alipokuwa akiwaleteaa mapochopocho toka mgahawani kwake. Hawakupungukiwa na pesa wala furaha. Akakumbuka pia siku ambayo alimwona mama yake na mwanamke mwingine akizipiga kavukavu mbele ya kadamnasi wakimgombania Kilonzo. Aliishika mkono kutoka kila upande wa mwili wake, akainyanyua na kuishusha chini. Akaikunja mikono yake kifuani, akapiga hatua moja kurudi nyuma.
“Ninaomba kazi.”
“Hata hii pia ni kazi tena itakulipa zaidi…” Naomi alitikisa kichwa na kumkazia macho Kilonzo.
“Nipe kazi ya kupika, kupiga deki au kazi ya kuhudumia wateja.”
“Kazi iliyopo ni kuhudumia moyo wangu….”
Naomi alipiga hatua moja tena nyuma. Hakubandua macho yake kutoka usoni kwa Kilonzo. Akashika kitasa na kubinjua.
“Acha kuchezea bahati wewe. Utabaki na umasikini wako… Naomi, Naomi?”
Naomi alitoka ofisini mle akiwa amekunja uso. Wateja walimsindikiza kwa macho. Alipotoka nje, alitembea kwa hatua za taratibu. Tumbo lilinguruma kwa njaa. Paji la uso wake liliwa linatiririka jasho kama maji ya mvua. Akiwa katika hali hiyo, alikatisha Mtaa wa Hekaheka.
Hatua za Naomi zilimfikisha kwenye banda la Mama Inno, mama lishe aliyependwa sana na vibarua wa ujenzi, makondakta, wapigadebe na wwengineo kutokana vyakula vyake muruwa vilivyouzwa kwa bei poa. Naomi alijibwaga kwenye kiti na kutupa uso na mikono yake juu ya meza. Kwa dakika chache alionekana mithili ya kiumbe asiye na uhai. Mama Inno alikimbia akavuta kiti na kuketi kando yake, akamwinua na macho yao kugongana.
“Kulikoni Naomi?”
“Sijala toka jana!”
“Laaa! Nilidhani ni makubwa zaidi, kumbe hilo?” Mama Inno aliamka na kupotelea kwenye jiko lake kwa dakika 5 hivi, kisha akarudi na sahani iliyojaa wali na maharage, akampatia Naomi achangamshe tumbo lake.
“Ninaomba unisaidie ajira…… Mama Inno” Naomi aliendelea kuongea huku anakula. “Niajiri, nipike na kuhudumia wateja wako.”
“Pole sana mwanangu. kama unavyoona sina kikubwa.” Mama Inno alimtazama Naomi kwa makini na kuendeleza, “Natamani nikusaidie lakini mtaji mkubwa sina….”
“Sawa tu mama. Hata kama usiponilipa vizuri, utanilipa vile mchango wangu utakavyoonekana katika kipato chako.” Naomi alisema badaa ya ukimya wa muda mfupi uliotawala kati yao. “Niko tayari kufanya kazi mama.” Naomi aliongezea.
“Basi nashukuru mwanangu. Kipato tutakachozalisha tutagawana.
“Ahsante mama.” Naomi alishukuru baada ya kumaliza kula chakula chote. Moyo wake ulipata matumaini japo tabasamu la unyonge liliendelea kutamalaki moyoni mwake. “Nashukuru mama.” Safari hii alikuwa anashukuru si kwa chakula tu bali pamoja na kupata fursa ya kujipatia riziki kwa jasho lake.
“Wala usiwaze mwanangu.”
Naomi alitalishukuru akaanza kazi mara moja. Jioni walipofunga aliaga na kuelekea nyumbani kwao. Mwanga hafifu wa kibatari ulimulika ndani ya nyumba yao. Mama Naomi alikuwa ameketi kwenye kigoda chake akiwa ameshika tama na mlango bado uko wazi.
“Aanh kumbe Naomi?” Mama Naomi alistaajabu kumuona mwanaye amechelewa kurudi hadi giza limeingia.
“Shikamoo mama.”
“Marhaba mwanangu” Mama Naomi aliitikia. “Kuna usalama huko ulikotoka?”
“Salama mama.”
“Habari za mihangaiko ya kutwa nzima?” Kama siku zote tu mama lakini angalau Mama Inno amenikubalia nijishughulishe kwenye biashara yake.
“Pole sana mwanangu, Mama Inno ni mtu mwema.”
“Ndio mama. Naamini hivyo.” Naomi aliitikia na kuingia chumbani kwake. Alijitupa kwenye kitanda chake cha teremka tukaze.
Nuru ilipoanza kuchomoza upande wa mashariki siku ya pili yake, Naomi aliamka hima na kuelekea nje kunawa uso. Baada ya dakika kadhaa alikwisha kujiandaa akaondoka kuelekea kwa Mama Inno. Mkono wake wa kulia ulishika kilambo chake cheusi chenye nguo zake. Aliagana na mama yake na hatua zake za haraka zilimfikisha mapema kwa Mama Inno.
“Shikamoo.”
“Marhaba mwanangu, nyumbani kwema?” Mama Inno aliongea na Naomi akiwa anaendelea kufutafuta meza yake kwa sponji. Naomi alijiandaa na kuingia jikoni. Moshi wa moto wa kuni uliwasha macho yake akawa anakohoa, macho yanatoa machozi na makamasi puani.
“Mmh pole sana.” Mama Inno alisema alipoingia na kuona jinsi moshi ukimzonga Naomi ambaye ilikuwa wazi kabisa kuwa hana uzoefu na kazi ile.
Hata hivyo, kadri siku zilivyosonga juhudi za Naomi kazini zidhihirika zikampa faraja Mama Inno. Wateja nao hawakufumba midomo yao. Kutokana na huduma nzuri ya Naomi pale mgahawani wateja waliongezeka kila siku. Kipato cha mgahawa kilizidi maradufu. Hakika Mama Inno alifurahi sana.
***
Ulikuwa ni muda ambao nuru inazidiwa na giza angani. Ndege nao walikuwa wanarudi kwa maringo kwenye viota vyao. Naomi alionekana akifanya usafi ndani ya mgahawa na kuvipanga vyombo mahali pake kama ilivyokuwa kawaida yake baada ya kumaliza kazi. Mama Inno alikuwa ameketi kwenye kiti chake plastiki huku akiwa ameshika kibegi kidogo mkononi mwake.
“Naomi mwanangu?” aliita.
“Abee mama……” Naomi aliitika akafika hima pale alipokaa Mama Inno amsikilize.
Mama Inno alimkabidhi Naomi kile kibegi.
“Looo!” Naomi alishangaa kuona anapewa kimkoba kile ambacho Hakujua kina nini ndani yake. Alipokifungua, ndani yake aliona pesa zilizopangwa kwa uzuri uliovutia macho. Naomi alijitupa miguuni mwa mama Inno na kusema,
“Nashukuru sana mama.” machozi ya furaha yalitiririka mashavuni kwake.
“Wala usiwaze mwanangu. Hili ni jasho lako kama ilivyokuwa mapatano yetu.”
Naomi hakuwa na la kusema. Alirudia tena kushukuru, “Asante sana mama.”
“Sasa naweza kuanzisha mgahawa wangu mwenyewe.” alisema kimoyomoyo. Apopiga hatua chache akielekea nyumbani, alibadili njia ghafla, akaelekea kwenye mgahawa wa Mzee Kilonzo.