Lazima nifanikiwe

Art Type: Short story
Artist Name: Cecilia Mgimbila

Titus alikuwa ameketi juu ya jiwe lililokuwa pembeni kidogo ya nyumba yao, aliwaza, “Kwa nini nyoka yule amgonge baba yangu?” Alihisi huenda kuna mchezo umefanyika. Alitamani angekuwepo wakati nyoka anamgonga baba yake. Hakika angemsulubu vikali kwani alikuwa ameondoa furaha iliyokuwepo kabla. Alimtazama mama yake aliyekuwa na tumbo kubwa lenye kiumbe ndani yake.
Mama yake alikuwa ameketi kwenye mkeka huku akiwa ameegemea ukuta. Titus alilinganisha jukumu lililokuwa mbele yake na umri wake wa miaka kumi na sita. Alitamani baba yake angekuwepo ashughulike nalo.
”Titus, Titus!” sauti ya Mama ilimtoa Titus katika lindi la mawazo.
“Titus!” Mama aliita tena.
“Naam!” Titus aliitika huku akishuka juu ya jiwe na kuelekea alikokuwa ameketi mama yake.
“Titus inabidi umkamate kuku mmoja ukamuuze.” aliongea Mama huku akiwa amepakata mikono yake na kumtazama Titus pima usoni.
“Kuku tena! Ndio mali pekee tuliyobakiwa nayo?”
“Ukichelewa tutampoteza ”
“Tutampoteza nani tena?” Mama Titus alitoa macho yake usoni mwa Titus na kulitazama tumbo lake huku akilipapasa kisha akayarudisha tena macho yake kwa Titus huku yakiwa na ukungu wa machozi. Titus aliinamisha kichwa chini huku akipepesa macho yake.
“Sawa mama.” Titus alisema na kuondoka kuelekea nyuma ya nyumba yao. Alikuta kuku watatu wakidonoadonoa na kuparuaparua ardhini. Aliwatazama kwa makini ili kujua yupi angeuzika kwa urahisi. Aliamua kumkimbiza jogoo mmoja ambaye alikuwa amenona. Jogoo aliingia na kunasa kwenye miiba. Titus alimrukia kama paka shume lakini jogoo alifurukuta akatoka na kumuacha Titus akiwa amejikwaa na kuangukia kwenye miiba.
“Aaaah asiii…!!!” aliguna Titus alipokuwa ananyanyuka na kuchomoa miiba mwilini mwake. Aliendelea kumkimbiza jogoo ambaye alipita kwenye vichaka vyenye majani makavu yaliyokuwa yakiurarua mwili wake kwa kuwa alikuwa amevaa shati ya mikono mi fupi na kaptura.
“Nikikushika nitakufundisha adabu”, Titus alisema akiwa amekunja ndita. Jogoo alikimbia na kuingia jikoni akajificha kwenye rundo la kuni zilizokuwa karibu na jiko la mafiga matatu. Titus alimfuata hukohuko jikoni, kufunga mlango wa bati lenye kutu. Alizisogelea zile kuni akaanza kuzipangua. Jogoo aliruka. Titus alimrukia na kumkamata mguu. Jogoo alipigapiga mbawa zake lakini Titus alimshika vizuri na kumbana mguu yote miwili akafungua kamba zilokuwa zimefungwa kwenye baadhi ya kuni kwa meno na mkono mmoja, mkono mwingine ukiwa umemfumbata yule kuku barabara kwapani. Alipomaliza kufungua, alitoka nje, akamuweka chini kuku na kumbana mbawa zake kwa mguu wa kushoto na miguu yake kwa mguu wa kulia huku akiendelea kuweka kamba vizuri iliamfunge.
“Ti, ti,titus!?” alisikia sauti yenye maumivu makali masikioni mwake. Titus aliamwachia kuku na kutimua mbio kuelekea mbele ya nyumba yao, alifika na kuanguka juu ya mkeka aliokuwa amekalia mama yake,
“Hah! hah! hah! mama, mama?” Titus alimwita mama yake huku akihema,
“Mh! Titus…!!!, kaombe-e…”Mama Titus aliongea akiwa anagugumia kwa maumivu. Alikuwa ameegemea mkono wa kushoto mmoja na kupapasapapasa tumbo na kiuno chake kwa mkono wa kulia,
“Ni, nikaombe nini?” Machozi yalimtoka Titus, akamkumbatia mama yake na kumhoji apata kujua nini kilimpasa afanye.
“Msaada mwanangu mmh! aahah!”
Titus aliutoa taratibu mkono wake mabegani mwa mama yake na kutimua mbio kuelekea akashika njia nyembamba iliyokuwa pembeni mwa nyumba yao na iliyosongwa na nyasi ndefu kiasi. Kwa mbali ilionekana nyumba ya msonge iliyoezekwa kwa nyasi. Mzee wa makamo alikuwa ameketi kwenye kigoda mbele ya nyumba hiyo. Kwa chini alikuwa amejifunga msuli na juu amevalia shati lafulana na koti la mikono mirefu; na baraghashia kichwani.
Titus alifika kwenye nyumba ile akihema. Titus alimshika yule mzee mkono akasema,
“Twendeehhh!”
“Wapi?” alihoji Mzee Jumbe huku akimtazama Titus kwa macho yenye viulizo vingi.
“Mama aaah, mama aaah, nyumbani!” Titus alikuwa akijibu huku akimvuta. Mzee Jumbe hakuongeza neon. Alimfuata Titus kuelekea kwao. Walifika nyumbani wakamkuta mama Titus jasho linamtoka, anagugumia akiwa ameuma midomo yake. Titus aliingia ndani na kutoa baiskeli.
“Shika vizuri.” Mzee Jumbe alimwambia Titus alipomuona akitoa baiskeli. Titus alikamata usukani wa baiskeli na kulibana Tairi la mbele kwa miguu yake.
Mzee Jumbe alimwinua Mama Titus taratibu, akamkongoja na kumpakia kwenye baiskeli.
“Njoo huku umshike.” Mzee Jumbe alisema akiwa ameshika kitako cha baiskeli kwa mkono mmoja na mwingine akiwa amemshika mama Titus. Titus aliutoa mguu wake taratibu kwenye tairi na kuachia usukani huku akiwa ameshika koti alilokuwa amevaa Mzee Jumbe. Alirudi nyuma taratibu akamwachia Mzee Jumbe ashike usukani na kuikokota baiskeli kuelekea zahanati.
Walipofika zahanati, Mzee Jumbe alimwagiza Titus aende mapokezi akamwite nesi. Titus alitimua mbio akaingia ndani akasimama mkabala na mlango wenye kibao kilichoandikwa MAPOKEZI. Alimkuta muuguzi aliyevalia gauni fupi la kijani aliyekuwa anafunuafunua karatasi zilizokuwa juu ya meza.
“Dada! Dada! kuna mgonjwa nje.”Titus alisema wa sauti ya juu huku akitweta kwa taharuki.
“Punguza sauti kuna wagonjwa wengine wenye maumivu zaidi yake.” alisema yule dada akiendelea kufungua karatasi. Titus aliangaza macho huku na kule lakini nakuona mgonjwa mwingine zaidi ya mama yake. Taratibu nesi alisimama na kufungua mlango na kutoka nje.
“Yuko wapi huyo mgonjwa mwenyewe?” aliuliza yule nesi akiwa ameshika kiuno.
“Yupo huku.” Titus alijibu akiwa amenyoosha kidole kuelekea aliokuwepo mama yake. Yule nesi akamfuata nyuma hadi mahali aliokuwepo mama Titus na mzee Jumbe.
“Pole kwa safari baba.” alisema yule nesi na kusogea moja kwa moja hadi alipokuwa Mama Titus. Alikuwa ameegemea ukuta na ameshika kiuno kwa mkono mmoja mwingine ukiwa unalisuguasugua tumbo lake.
“Asante mama.” alijibu Mzee Jumbe.
“Njoo tusaidiane kumuingiza ndani.” aliongea nesi akiwa anajaribu kumkongoja Mama Titus. Mzee Jumbe alisaidiana naye wakaenda naye hadi kwenye mlango wenye kibao kilichoandikwa WAZAZI. Waliingia ndani Titus akifuata nyuma. Ndani ya chumba kulikuwa na chumba kingine kilichoandikwa LEBA. Ndani kulikuwa na kitanda cha chuma na godoro lililoisha lililokuwa limetandikwa shuka kuukuu jeupe. Walimkalisha Mama Titus kitandani kisha nesi akasema,
“Mzee unaweza kwenda nje.”
“Sawa mama.” alisema Mzee Jumbe akatoka nje.
“Na wewe unasubiri nini? Naenda nje.” nesi alimwambia Titus kwa ukali. Titus aliinamisha kichwa chini na kutoka nje. Alimkuta Mzee Jumbe akiwa amekaa juu ya jiwe lililokuwa chini ya mti nje ya zahanati,
“Titus njoo.” Mzee Jumbe alimwita kwa sauti na kwa ishara kwa mkono. Titus alisogea taratibu akiwa ameinamisha kichwa chini. Mzee Jumbe alimshika mkono na kumvuta aketi karibu naye.
“Mama atakuwa salama usiwaze. Halafu wewe ni mtoto wa kiume, jikaze.” Mzee Jumbe alimfariji Titus huku akimpapasa mgongoni. Titus alitikisa kichwa, akafuta machozi yaliyokuwa yakimbubujika.
“Acha mi niende nyumbani nitarudi muda sio mrefu.” Mzee Jumbe alisema akasimama. Titus alitingisha kichwa lakini hakumjibu. Mzee Jumbe Alipanda baiskeli na kuondoka huku Titus akiwa kimya, anamtazama.
Titus akiendelea kusubiri. Nusu saa baadaye alimwona nesi akitoka akiwa anatoa mipira aliyokuwa amevaa mikononi na kuitupa ndani ya ndoo ya taka. Titus alinyanyuka na kumfuata nesi ili aulizie hali ya mama yake. Nesi aliingia moja kwa moja hadi kwenye chumba cha mapokezi. Titus alimfuata na kumuuliza,”Naruhusiwa kumuona?”
“Bado. Kwanza kamwite baba yako.” alijibu yule nesi kwa mkato.
Kwa unyonge Titus akajibu, “Hayupo.”
“Kaenda wapi?”
“Alishafariki.”
“Ns yule uliyekuja nae ni nani?”
“Ni jirani yetu.”
“Hee makubwa! Sasa pesa anatoa nani?” Nesi alihoji akiwa ameshika kiuno.
“Hela ya nini?”
“We mtoto, sihitaji maswali.”alisema yule nesi akimnyooshea kidole Titus ambaye alikuwa anamkodolea macho tu pasipo kuwa jibu la kumpa.
“Kimbia kawaambie ndugu zako inahitajika elfu sitini sasa hivi.”
“Ya nini?” aAlihoji Titus kwani Hakujua kiasi kikubwa hivyo cha pesa ni cha nini na angekipata vipi.
“Sihitaji maswali fanya nilichokwambia.” alifoka yule nesi.
“Asa wakiniuliza ya nini niwaambiaje?” Titus aliendelea kuhoji akiwa amemkodolea macho ya ghadhabu na taharuki nesi yule,
“Nenda kawaambie ndugu zako inahitajika hela kwa ajili ya vifaa vya kujifungulia mama na hela ya kitanda kwa sababu atatakiwa kukaa hapa kwa muda baada ya kujifungua, haya nenda upesi.”
“Lakini…!!!”
“Lakini nini?” nesi alimkata kauli.
“Akina mama wajawazito na wazee wanapatiwa huduma bure.” Titus alikomaa.
“Nani kakwambia? Nenda kachukue hela acha kufanya mzaha.”
“Mi nilisikia redioni.”
“Ukiendelea kubisha utampoteza mama yako bure. Fanya hima.” Titus alilia aliposikia maneno ya kifo. Alipiga magoti na kushika pindo ya gauni la nesi.
“Nakuomba umsaidie mama yangu nesi mi sina hela.”
“We hebu niache!” alisema nesi huku akmvuta gauni lake lililokuwa limeng’ang’ania mikononi mwa Titus.
“Lakini mama yangu anapaswa kutibiwa bure.”
Nesi alimtazama Titus na kubetua midomo yake.
“Mama yangu lazima atibiwe haiwezekani.” Titus aliendelea kulalama.
“Sipendi kubishana na vitoto. Toka ukapigie kelele huko nje.” nesi alisema na kumsukuma akimsukuma Titus. Titus alipepesuka akajivuta pembeni huku anatokwa na machozi.
“Wajawazito wanatakiwa kutibiwa bure, usitoe wala kudai fedha, Hivyo ndivyo nilivyosikia radioni.” Titus aliendelea kumuelimisha nesi yule. Hakutaka kumpa nafasi ningine ya kuzungumza. “Mama yangu akifa…” alionya lakini hakuweza kumalizia sentensi. Aliangua kilio huku akimtazama nesi kwa hasira. Nesi alimtazama Titus na kuingia kwenye chumba cha leba. Titus aliendelea kuzungukazunguka pale nje ya mlango wa chumba cha leba akiwa ameshika kichwa na machozi yakiendela kumtoka kama matone ya mvua.
Hatimaye Mzee Jumbe akirejea na mfuko mweusi. Alipomtazama Titus aligundua huzuni aliyokuwa nayo.
“Titus shida nini, vipi hali ya mama?”
Kimya.
Taratibu Titus alifungua mdomo na kusema, “Nataka nisome nije kuwa daktarin.”
“Ni wazo zuri, hakika utafanikiwa.” Mzee Jumbe alimfariji Titus, akafanikiwa kuliona tabasamu lake.

Gallery

Share the Post: