Msitu wa Ajabu

Art Type: Short story
Artist Name: Irene Magayane

Ilikua asubuhi. Jua lilichomoza upande wa mashariki mwa kijiji cha Mwendapole mithili ya macho ya mtoto mwenye hasira kali; na kupenya kwenye nyufa za nyumba ya udongo waliyoishi Rebeka na mama yake.
“Rebeka?”
Kimya!
Rebeka aliyekuwa amejilaza kwenye mkeka kama mzigo wa kuni aliupuuza wito wa mama yake. Mikono ya mama yake iliishika miguu yake na kumtikisa. “Wewe, hebu amka!”
Rebeka alikurupuka na kutupa shuka alilokua amejifunika, lililopambwa kwa viraka vilivyochakaa. Alisogea dirishani na kuchukua jagi na kijti alichotukimia kama mswaki na kuelekea uani. Alisugua meno hadi fizi zikatoa damu. Sauti ya mama ikapasua tena anga kwa ukali.
“Wewe, unachelewa shule!”
Rebeka alimpotezea mama yake na kutembea kwa mwendo wa kinyonga kuelekea ndani.
“Sioni sababu ya kwenda shule mama.” alilalamika.
“Kwa nini?” Mama alifoka huku akimkazia sura.
“Kila mara narudishwa tuu! Mara viatu. Mara soksi. Mara madaftari.” Aliendelea kulalama.
“Leo si una mitihani wewe?”
“Mitihani yenyewe kila siku nafeli, sasa si bora tu nisiende. Kwa nini niendelee kuteseka? Mimi nimechoka sasa.” alijitetea Rebeka huku akipandisha na kushusha mabega yake.
Paaaaaah! Kofi la nguvu kutoka kwa mama yake lilimkurupusha Rebeka. “Haya, potea, nisikuone hapa!” alifoka mama Rebeka.
Rebeka alivaa shati lake lililofubaa na kuishikiza vizuri sketi yake kiunoni kwa pini. Alivaa soksi zake zilizopwerepweta na kuingiza miguu yake kwenye viatu vyake mchubuko vilivyojaa matobo. Alichukua mfuko wake wa madafari na kutoka nje kuelekea jikoni kujipatia staftahi. Kwa kuwa alikuwa amechelewa, alifungasha gimbi kwenye jani la mgomba mama yake alilomtengea kwa ajili hiyo. Alianza safari ya kuelekea shuleni na kumuacha mama yake akilima pembeni mwa kibanda chao.
Rebeka alikatisha mitaa ya kijiji cha Mwendapole. Miti ya miembe iliyositawi kwenye kingo za njia ilikuwa imechanua maua yenye harufu nzuri ya kuvutia. Ndege waliimba kwa sauti za shangwe kuipokea asubuhi angavu. Rebeka aliburuza miguu yake taratibu huku akipiga changarawe zilizopo njiani kama mpira. Alisikia minon’gono ya watu nyuma yake na kugeuza shingo yake kuwatazama. Lilikuwa ni kundi la wanafunzi wenzake likiongozwa na Riziki. Rebeka alijisogeza kando ya njia ili kuwapisha. Walipomfikia, Riziki alimvuta shati lake na kumsukumia mbali huku akimbinulia midomo na kufyonza huku wenzake wakimcheka.
Moyo wa Rebeka ulijawa na uchungu, alihisi kuna kitu kimemkaba kooni. Alimiminika machozi. Alijichukia, akajiona hafai katika dunia. Rebeka alijinyanyua kwa haraka na kukimbilia porini akijua fika kwenye pori hilo hakuna usalama. Alirandaranda ndani ya pori lililosheheni nyasi ndefu na fupi za kila aina. Alikua tayari kwa lolote. Bora nikutane na wanyama wakali kuliko binadamu. Alijisemea mwenyewe huku akifungua mfuko kutoa gimbi ili apooze njaa.
Rebeka akiwa anaendelea kupuyanga, alisikia sauti ikiishia hewani. Akatega sikio lake huku akiangaza macho huku na kule ili ajue sauti ile ni ya nani. Alipogeuka, alistaajabu kumuona bibi kizee akiwa anajigalagaza kwenye nyasi huku akipiga miayo na kuhemea juu juu kama mtu aliyebanwa na pumu. Alifungua mfuko taratibu na kurudisha lile gimbi kisha akajifutafuta mikono yake iliyokua na vichenga vya gimbi. Alipomkaribia yule bibi, aliangalia pembembeni na kuanza kuimba imba, huku akishikashika majani. Akampita yule bibi kana kwamba hakumuona. Moyo wake ulisita huku akijiuliza, ”hivi kwa nini nisimpatie bibi hili gimbi? Anaonekana ana njaa kuliko mimi, lakini hapana. Kama ingekua kweli si anganiita? Huruma zilimponza fisi, atajijua mwenyewe. Kwani kaniona?”
Nafsi yake iliendelea kumshutumu, akajikuta akirudi nyuma. Akaingiza mikono yake tena ndani ya mfuko na kutoa kipande cha lile gimbi kilichokuwa kimebakia, akampatia yule bibi. Bibi alipokea kwa mikono miwili huku akitetemeka na machozi kumlengalenga.
“Kwa heri bibi.” Rebeka aliaga, akaendelea kuzurura ndani ya msitu ule bila mwalekeo.
Aliangaza macho huku na kule na kuona miti na nyasi za kila aina. Ndege wa rangi rangi waliruka juu ya miti na kushangilia. Mh! Ghafla, Rebeka alishtuka na kurudisha fikra nyuma. Huu si ndio msitu wa ajabu unaosifika kuwa una wanyama wakali hapa kijijini? Alijisemea kimoyomoyo, lakini aliendelea kujipa moyo. Nitapita kando kando, wala sitaukaribia. Alishusha na kupandisha pumzi.
Mara sauti za ndege zilibadilika na kua zisizo za kawaida. Sharaaa! sharaa! Upepo nao ulivuma kwa kasi ya ajabu. Wbhuuuuuu! Majani ya miti yalipepea kama bendera na kuifanya ile sehemu kuwa ni ya kipekee. Rebeka alihisi nywele zikimsimama kichwani. Ngozi yake iliota vipele, mwili ukatetemeka kama ardhi iliyopatwa na tetemeko. Yani leo nimekwisha. Alijisemea Rebeka akiwa amehamaki asijue la kufanya.
Ukimya ulitawala pande zote kwa sekunde kadhaa; kisha ghafla, sauti nzito zilisikika zikinong’ona kama spika iliyoharibika. Nyasi zililala na kunyanyuka. Matunda ya miti yakabadilika rangi, na kila tunda likaanza kutoa rangi yake. Manjano. Urujuani. Nyeusi. Samawati. Rebeka kajiuliza, “nilipotoka ni mbali, na ninapoelekea sipajui, je nirudi kweli? Hapana, nitajikaza kisabuni, japo sijui kama nitatoka salama.” Alipiga moyo konde, akaendelea kusonga mbele.
Mara paap! Yule bibi alitokea mbele yake akiwa anatabasamu kwa furaha ya ajabu huku akionyesha meno yake yaliyochongoka kama mshale. Sura yake iling’aa kama kioo na macho yaliangaza kama tochi. Nywele zilionekana nyeupe kama povu la sabuni. Gauni lake ilipambwa kwa magome ya miti. Kucha zake za mikono zilimeremeta mithili ya mapambo ya harusi. Viatu vyake vilipambwa kwa ngozi ya chatu.
“Mamaaaaaaaaaaa!” Rebeka alipiga kelele kwa nguvu na kuangusha vitu vyake alivyokuwa ameshika. Mwili wake ulijawa na uoga wa ajabu. Mapigo ya moyo yaliongezeka. Macho yakamtoka. Miguu ikafa ganzi kama mtu aliyepigwa na shoti. Aliweweseka na akili yake kuvurugika, akahisi kama anaota. Sauti ilimkauka kooni mwake. Alitamani kukimbia, lakini alishindwa, kwani miguu yake iling’ang’ania kwenye ardhi. Mara, wingu zito likatanda na radi zikamulika huku na huko. Ngurumo na upepo mkali vikarindima.
“Usiogope mjuukuu wangu, hakuna baya litakalokutokea. Nitakuwa pamoja na wewe mpaka mwisho wa safari yako.” Rebeka alisikia sauti ya mtetemo ya bibi yule iliyojirudia kama mwangwi. ”usiogo…..ogo….pee…pee…mjuk…uku…uuu” huku akimsogelea. Rebeka hata hakuelewa maana alikuwa ameshavurugwa na yale mambo aliyoyaona. Alianza kurudi kinyumenyume.
Bi Kizee aliendelea kumsemesha, “nimekuletea zawadi mjukuu wangu ila hii zawadi ina masharti sharti lake. Hutakiwi kuiacha mahali popote. Kila mara tembea nayo ishikilie, usipofanya hivyo utajikuta unapata taabu sana”.
“Sa….aa..wa.. bi..bi” alijibu Rebeka huku anatetemeka.
“Kwaheri mjukuu wanguuuu” sauti ilishiia, na upepo ukatoweka vuuuuuu! Wingu zito likatoweka pia na hali ikawa shwari.
Kutazama mbele yake alipokuwa ameketi yule bibi, Rebeka alistaajabu kuona kitabu kikipepea.
“Mmhh! Hiki ni nini? ” alijiuliza huku akiwa anakitazama kwa uoga. Rebeka akataka kukimbia, lakini moyoni mwake akawa anasikia sauti “chukua hicho kitabu”. Rebeka alisita. Suti ikarudia mara tatu, ”chukua hicho kitabu.” Rebeka akainama na kunyoosha mikono yake, akajaribu kukigusa kile kitabu, kisha akairudisha akiwa hana hakika anapaswa afanye nini. Akapiga hatua mbele lakini anarudi tena, akainama akakishika kwa kutetemeka.
Baada ya kushika kile kitabu, akili zake zinarudi akaendelea na safari. Sasa akafika ndani ya ule msitu ambako ndipo kwenye njia ya kutokea ng’ambo ya pili. Ghafla akafungua kile kitabu akahisi kuna nguvu fulani hivi. Rebeka akaastajabu ile hali ya kujawa na ujasiri aliyokuwa nayo ghafla. Msituni akastaajabu kuona wanyama wakali, kama simba na chui wakimtolea macho makali, wanaguruma huku wakipiga miayo.
Rebeca alianza kuhoji ujariri wake mbele ya wanyama wale hatari alikumbuka yale maneno ya Bi Kizee,
“Mjukuu wangu usiogope kwani hakuna lolote baya litakalokutokea. Ntakuwa pamoja na wewe mpaka mwisho wa safari.”
Rebeka akafungua kile kitabu. Mara wale simba na chui wametoweka mbele ya macho yake.
“Hee wameenda wapi?” alijiuliza Rebeka akiwa anastaajabia masaibu aliyokuwa akinayashuhudia. Mbele kidogo anakutana na vichaka vingi na kuona ndege wakiwa wanachukua majani mdomoni na kuyaweka kwenye viota vyao.
“Mhh mbona sioni njia.” Rebeka akajiuliza akiwa anatamani kuimaliza safari yake isiyokuwa na mwelekeo. Aliendelea kutembea vichakani akipapasa kuna kama kuna njia iliyoota majani. Alipofika mbele kidogo aliona njia. Kwa mbali akaona maandishi ya kibao cha shule.
“Hapana, siamini kama nimefika shuleni!” alijisemea huku akipepesa macho yake huku na huko. Nyuma yake alihisi kama kuna watu wanamtazama. Kugeuka aliwaona wale wanaafunzi alikuwa amekutana nao awali.
“Kumbe mlikuwa hamjafika shuleni” aliuliza.
“Achana na sisi bwana. Endelea na safari zako. Wewe si umejidai kutupita pale msituni? Subiri uone yatakayokupata. Utajuta!” alisema Neema huku akiwa anamvuta mkono Zainabu ili wakimbie, wamuache.
Hatimaye Rebeka akafika shuleni akakuta kimya!
“Tobaaaaaaaaaa! Nitasema nini leo mtihani nimechelewa, sina ninachokijua, fimbo napigwa, sijui itakuwaje!”
Mara akakumbuka yale maneno ya bibi. akafungua kile kitabu na ghafla kujikuta darasani. Wanafunzi wote wakamtazama kwa mshangao, “Huyu kaja saa ngapi? ” kila mtu alimuuliza mwenzake. Punde si punde mwalimu akaingia.
“Hamjambo?”
“Hatujambo shikamoo mwalimu.”
“Marhaba, haya kaeni tayari kwa mtihani.”
“Leo tutafanya mitihani mitano na kila mmoja asipate chini ya 70% kwa kile somo. Mmenielewa?”
“Tumekuelewa mwalimu.” walijibu wanafunzi wote kasoro Rebeka.
Mwalimu akamhoji, “We mbona hujibu?” watu wote wakaangua kicheko.
“Mwalimu huyo nd’o alivyo. Hajawahi kupata maksi za juu kiasi hicho. Yeye kila siku maksi zake ni namba za viatu.” alijibu Neema kwa kujiamini.
Rebeka alibaki kimya. Waliambiwa waweke kila kitu nje kwa ajili ya mtihani.
Rebeka aliwaza, “nimepewa sharti moja tu hiki kitabu nisiweke chini itakuwaje nikikiacha nje?”
“Fanyeni haraka msipoteze muda.” mwalimu alihimiza.
Wanafunzi wote wakaacha matini yao wakaingia darasani kasoro Rebeka.
“Hivi wewe mtoto una matatizo gani? ” mwalimu aliuliza.
Mwanafunzi mmoja akadakia na kusema, “anasubiri chabo huyo”.
Huko nje Rebeka akawa anajiuliza afanyeje. Akakumbuka ile sauti ya Bi Kizee, “Usiogope mjukuu wangu hakuna lolote baya litakalokutokea.Nitakuwa pamoja na wewe mpaka mwisho wa safari.” Akaweka kitabu chini akapiga hatua moja mbele. Ghafla zile sauti za msituni zikamtokea. Akaanza kuweweseka. Akakumbuka tena kauli ya pili ya yule Bi Kizee, “Hii zawadi ina sharti moja. Ishikilie usiiache. Ukiiacha utapata taabu sana.” Harakaharaka akarudi nyuma, akainama akakishika kile kitabu. Akaingia, akasogea mbele ya mwalimu ili amruhusu kuingia nacho ndani kwani kiliandikwa maneno mawli tu.
Mwalimu akimkazia macho kwa ukali.
Rebeka akaanza kutaka kujieleza, “Mwali….”
Alikatishwa. “Rudi nje.” alisema mwalimu.
“Hapana Mwalimu nakueleza ukweli.”
“Ukweli upi?”
Rebeka akaanza kufungua kile kitabu ili amuonyeshe mwalimu. Ghafla akajikuta akiwa amekaa kwenye kiti anafanya mtihani. “Mmmmmh! Nimefikaje hapa? Inamaana mwalimu hajakiona hiki kitabu?” Rebeka alijiuliza mwenyewe kimoyomoyo.
Mwalimu akaanza kugawa karatasi za mitihani. Rebeka alipofungua karatasi za mtihani wa kwanza, “Mmhh! Mbona mtihani wa leo kila swali naweza kulijibu?” alijuliza moyoni mwake. Wa pili kadhalika, hadi wa tano
“Haya nyote wekeni kalamu chini. Wanafunzi wote wakaweka kalamu chini mwalimu akakusanya karatasi za mtihani, kisha wote wakatoka nje; kila mtu akiwa anakuna kichwa isipokuwa Rebeka.
“Yaani mtihani wa leo sijui Rebeka atapata nini kama sio yai.” alisema Zainabu.
Rebeka alipata ujasiri wa kuwasogelea wanafunzi wenzake waliokuwa wakijadiliana kuhusu mtihani pale nje ya darasa, akiwa na kile kitabu chake mkononi.
“Yaani leo mtihani ulikuwa rahisi sijawahi kuona.” alijisemea Rebeka huku akifungua kile kitabu. “Mnaona hiki kitabu?” aliwauliza na kuwaonyesha wenzake.
“Huyu kachanganyikiwa jamani kitabu kiko wapi mbona hatukioni!” alidhihaki Riziki.
Siku mbili baadae mwalimu aliingia darasani akauliza, “Rebeka, huu mtihani umefanya mwenywe?”
“Ndio Mwalimu.” Rebeka hakuelewa kwa nini anaulizwa swali lile na hali mwalimu mwenyewe ndiye aliyesimamia mtihani.
”Umepata maksi nyingi kuliko wote katika masomo yote matano.”
“Aaaaaaaaaaannh!” wanafunzi wenzake wakabaki midomo wazi.

Gallery

Share the Post: