Hatima ya Mtemi
“Hapana sikubali kukosa kama ilivyokuwa wiki jana.” alilalamika mmoja kati ya wananchi wa Songambele waliokusanyika mbele ya nyumba ya mtemi huku wengine wakisukumana. Kila mmoja alikuwa ameshikilia mfuko wa kubebea chakula. Haikupita muda mtemi Kasansa alifungua mlango alitoka nje. Aliwaangalia wananchi wake kisha akatabasamu kidogo. Sura yake yenye makunyazi, ndevu nyeupe na macho yaliyofififia ulitosha kuwafanya wananchi kuwa watulivu.
Mtemi alikaa kwenye kiti kilichowekwa mbele. Wale wananchi walipiga makofi mara mbili kisha waliinama kutoa heshima kwa kiongozi huyo mkongwe.
“Tumekusanyika hapa ili tugawane kile kidogo tulichobakisha katika hazina yetu.” aliinua glasi ya maji na kunywa kidogo kisha akaendelea). “Leo tutanza na wale ambao hawakupata katika mgao uliopita.” mtemi alimalizia kauli yake.
“Hapana haiwezekani. Kwanini tusi….?” minong’ono ilienea kila kona baina ya wananchi kwani hakuna aliyekuwa na chochote cha kuweka tumboni kati yao.
“Koroma wagawie chakula.” mtemi alimuamuru mkewe huku akinyanyuka, akachukua fimbo yake na kuingia ndani.
“Naombeni mtulie. Akinamama wenzangu kaeni chini.” mke wa mtemi alisema huku akiendelea kugawa chakula. Hawakupata zaidi ya wananchi kumi wa mwanzo. Chakula kingine kikimwagika chini kutokana na vurugu za wananchi.
Koroma alisimama kwa ghadhabu kisha alielekea ndani kwa mumewe. Wanyapara walisogea karibu huku wakisubiri amri kutoka kwa mtemi juu ya nini cha kufanya na wananchi wale.
“Fanya haraka! Tupite huku….” wananchi walisemezana na kuondoka hima katika himaya ya mtemi, wakatokomea katika vichochoro huku watoto wao wakiwafuata mithili ya vifaranga vya kuku.
“Nilikuambia mke wangu huu sio uongozi! Umeona? Ni mara ngapi mzee mwenzangu ameambiwa aachie usukuni lakini anakataa?”
“Ghala limejaa jasho letu. Tumelima wenyewe. Tumekusanya na kuingiza ghalani lakini…., hapana mke wangu hatuwezi kufumbia macho tena suala hili!” Mzee Kasagama alimwambia mkewe wakiwa nje ya nyumba yao.
“Japhari! Japhari !”
“Naam baba.” sauti ya mtoto wao ilisikika akiitikia kutoka ndani.
“Njoo mwanangu. Njoo na mdogo wako.” Mzee Kasagama alisema huku akimuangalia mkewe aliyekuwa anapumua kwa shida ilhali amelipakata lake tumbo katika mapaja yake.
“Kwa, kwa, kwa.” Japhari alitembea akiongozana na mdogo wake Shomari kuelekea nje, kando kidogo ya nyumba yao, alipokuwa amejituliza mzee jioni ile. Walipofika waliketi. Kasagama alikoleza moto kwenye kiko kilichotulia imara katikati ya midomo yake. Akavuta moshi puani na kuutoa nje kupitia kwenye vipenyo pembeni mwa midomo yake. Akapiga chafya na kuvuta moshi tena. Safari hii akautoa nje kupitia puani, kisha akaanza kuzungumza,
“Wanangu sasa mu wakubwa. Baba yenu nimezeeka. Naye mama yenu ana ujauzito kama mnavyomuona. Ndani hakuna hata ganda la kiazi. Alivuta pumzi kidogo kisha akaendelea. Nnendeni katika ghala la mtemi wanangu mkachukue chochote tunachoweza kuweka tumboni. Vinginevyo, njaa hii itatumaliza.”
“Lakini baba….”
“Hakuna cha lakini mwanangu Japhari. Leo ni siku ya tatu matumbo hajapokea chochote. Fuata ninachokuambia. Cha msingi muwe makini wanangu. Sawa?” mzee alinena kwa sauti ya kukoroma.
Vijana wale hHawakuacha kunong’ona kwa hofu waliyokuwa nayo. Mwishowe walilala wakisubiri kiza kitande.
“Kaka, kaka, amka!” vijana waliamshana kwa kunong’ona
“Kokorikooh!” Jogoo naye aliwakumbusha kuwa walipaswa wafanye haraka kwani karibu kungepambazuka.
Vijana wale walifungua mlango na kuanza safari kuelekea kwa mtemi.
“Ta! ta! ta! ta!” walinyata wakajipenyeza na kuingia katika ghala pasipo wanyapara kujua.
***
“Kaka tuondoke!” Shomari alimkonyeza kaka yake baada ya kufungasha mizigo wa kumtosha kubeba; kisha “chwaaaaaa!” Shomari alifyatuka mithili ya upepo kutoka katika ghala akaenda kujificha katika jengo jirani akimsubiri kaka yake.
“Huu mwanga unatoka wapi? Duu wameamka nini?” Japhari alijisemea kimoyomoyo akiwa bado ndani ya ghala.
“Ndu! Ndu! Ndu!” vishindo visikika vikielekea kwenye ghala. Japhari aliuacha mzigo wake na kujaribu kutoroka.
“Pa!pa!pa! pa!pa! pa!” mishale ilimkosa. Aliruka na kujibanza ukutani.
“Pita kushoto hayuko mbali huyu leo lazima akipate cha mtemakuni. Hatumuachi!” walinzi walinong’onezana.
Japhari na mdogo wake walitimua mbio mithili ya swala waliojeruhuiwa huku walinzi wakiambulia vumbi na kuokota viatu chakavu vya watoto wale.
“Nawafahamu hawa ni watoto wa nyumba ya tatu lazima tuwasulubu tu!” aliapa mmoja wa walinzi wale.
Japahari na mdogo wake walizama ndani nyumbani kwao pasi na hodi, huku wakitweta.
“Japhari kuna usalama mwanangu?” Kasagama alikoroma huku akikurupuka toka kwenye usingizi wa mang’amumang’mu.
“Aaanh, hamna baba.”
“Mmerudi nyote?” mzee aliuliza tena, huku akijizoazoa kuelekea mlangoni. Walisimuliana harakaharaka kilichojiri wakaingia ndani na kukomea mlango.
“Laah! Poleni wanangu. Tulieni ndani, hata waje hao walinzi hatoki mtu hapa ndani.” mzee alihitimisha mazungumzo na wanae akarudi chumbani kumtuliza mkewe.
***
“Juma ulisikia tangazo la jana?”
“Ah! Mimi sitaki kabisa kusikia habari za mikutano ya mtemi.”
“Hapana Juma, walisema asikose hata mtu mmoja katika….”
“Acha habari hizo.” Juma alijibu huku akipiga hatua kuondoka, kisha alisimama tena.
“Wewe unaongelea mikutano, unajua Japhari na mdogo wake wako wapi? Vijana tuamke ni muda wa kuleta mabadiliko sasa.” Juma alijibu na kuwasikiliza vijana wenzake wakihamasishana chini ya mti wenye kivuli. Waliamua kwenda mkutanoni kuona kitakachojiri.
***
“Wanamaendeleo mpo?”
“Tupoo!”
“Kama nilivyowajulisheni, tumekusanyika hapa kwa jambo moja tu, nalo ni juu ya hawa vijana waliovunja sheria za kijiji chetu cha Songambele.” Mtemi alitulia kwa muda kisha akaamuru wanyapara watulize minong’ono ya wananchi. Halafu aliendelea, “Kama ilivyo sheria ya kijiji chetu, vijana hawa wamepata hukumu ya kifo ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia mbaya kama wao.
“Sihitaji kuona mnayoosha mikono. Hili halina mjadala.” alifoka Kasansa baada ya kuona vijana na mzee Kasagama wakiwa wamenyoosha mikono juu.
“Rudi nyuma, rudi nyuma, pita kushoto, kimbia kule haraka.” wanyapara walijipanga baada ya kuona vijana wanaanzisha vurugu.
“Njooni haraka haiwezekani! Leo ni leo!” vijana waliitana huku wameshikilia mawe na fimbo. Mkutano ulivurugika na Mtemi akatoweka katika eneo lile mithili ya nyoka anavyoteleza pangoni.