Tabu Tabuni

Art Type: Short story
Artist Name: Otilia Angelus Haule

Mwalimu aliita kwa sauti ya ukali, “Tabu huu ndio muda wa kuja shuleni?”
“Hapana mwal….”
“Hii shule ya baba’ko?” alifoka huku akimtazama Tabu. “Ni mara ngapi nimekusamehe? Sitaki tena kusikia kelele zako!” mwalimu aliendelea kufoka huku akigeuka na kuangalia ubaoni. Mwalimu alipogeuka Tabu alirudi kinyumenyume kuelekea kwenye kiti chake. Mwalimu aligeuka ghhafla, “Unaenda wapi?” aliuliza huku akimfuata, uso wake akiwa ameukunja kama amekula ndimu. Alimkaribia Tabu. Tabu akaingiwa na wasiwasi, alijikuna kichwa, kisha akauma vidole vyake na kuendeleza kurudi kinyumenyume.
“Nilikwambia utoke nje, hukunisikia?” mwalimu aliongea na kumvuta Tabu shavu, akalivuta akiwa anampeleka nje. Tabu alikunja uso kwa maumivu, huku mkono wake wa kulia ukijaribu kuusukuma mkono wa Mwalimu wake utoke shavuni kwake. Walipofika mlangoni mwalimu alimsukuma Tabu nje akarudishia mlango na kusema, “Piga magoti hapo nje mpaka nitakapotoka.”
Machozi yalimbubujika Tabu akajiona hana thamani tena. Alijutia hali ile kwani alikuwa hafanyi kwa makusudi kuchelewa. Alikata tamaa kabisa ya kusoma na hakujua cha kufanya. Saa moja ilipita Tabu alikuwa amepiga magoti anamsubiri mwalimu wake amuamulie hatma yake. Mlango ulipofunguliwa, mwalimu kutoka nje. Machozi yalimtiririka Tabu alipotia tena machoni. “Stupid kabisa! Tena unyamaze utulie kama maji mtunguni. Kweli aliyekupa hilo jina hakukosea.” mwalimu alisema huku akimpigapiga Tabu kichwani. Tabu alinyanyua macho yake na kumtazama mwalimu wake usoni. Macho yake yalikuwa yameiva na kuwa mekundu kama nyanya. Matundu ya pua yaliyofunuka kama ya nguruwe yalimfanya Tabu aogope zaidi. Hata hivyo alijikaza na kusema;
“Mwalimu naomba unisamehe! Nisamehe, nisamehen nisamehe! Nitajita….”
Mwalimu alimkatisha, akavuta kitambaa kidogo kutoka kwenye mfuko wa suruali yake na kumuinamia Tabu, akamshika bega kisha akausogeza mdomo wake karibu na sikio la Tabu. “Leo utapata adhabu kali zaidi. Hivi ninavyoongea hapa nyanyuka ukajaze kokoto kwenye chumba kile cha darasa.” Mwalimu alisema huku akionyeshea jengo lililokuwepo pembeni kabisa na waliopokuwepo. Wanafunzi walionekana wanachungulia madirishani na wengine walitoka nje kushuhudia kinachoeldelea. Wapo waliokuwa wakicheka na wengine walihuzunika. Tabu hakuyajali yote hayo alinyanyuka akakatisha kwenye mti wa bendera. Akaiacha ikipepea bila kuitupia jicho, akakunja kulia na kukutana na jengo lililoning’ninizwa kengele, akaingia ndani. Mwanga hafifu uliokuwemo ndani mule ulimfanya ashindwe kuona vyema. Baada ya dakika mbili Tabu alitoka na ndoo mbili pamoja na jembe.
Safari ya kuelekea machimboni ilianza. Hapakuwa mbali na shule yao ila ugumu ulikuwa kupandisha kilima kile cha Sedure. Mashimo na mawe makubwa ndiyo yaliyoonekana hapo. Kulikuwa na watu, wake kwa waume walichakarika kuponda mawe. Magari makubwa kwa madogo yalionekana yakitoka na kuingia kwa ajili ya kubeba kokoto. Tabu aliangaza macho huku na huko akitafuta sehemu yenye mabaki ya kokoto na mawe madogomadogo. Haikuchukua muda Tabu alipata sehemu nzuri yenye kokoto kubwa na ndogo. Alifanya kazi kama siafu ili aweze kumaliza na kurudi nyumbani. Kazi ilikuwa ngumu sana. Tabu alionekana kuchoka. Mikono yake ilitoka malengelenge. Jasho lilmtoka kwa wingi na njaa ilimuuma sana lakini hakuwa na lakufanya. Nguvu zilimwishia na kushusha pumzi kwa nguvu;
“‘Mmmh!’ Eenh Mungu nisaidie. Nitaweza kupandisha hizi ndoo kweli?” alisema kwa sauti huku akitazama viganja vya mikono yake na nguo zake za shule zilizojaa vumbi.
Machozi yalimlengelenga. Alinyanyua ndoo na kuanza kupandisha kilima, alipepesuka huku na huko. Makorongo, visiki, mashimo na mawe makubwa vilikuwa vikwazo vya safari yake. Saa kumi na moja kamili ilimkuta bado akiwa kwenye eneo la shule, alijaza kokoto. Hatimaye aliamua kurudi nyumbani.
Safari ya kuelekea nyumbani ilikuwa ndefu, nayo ilizidi kumchosha kabisa. Alitembea kama kinyonga huku ameubana vyema mfuko wa madaftari kwapani. Matukio yote yaliyotokea mchana alikuwa kama kivuli tu.
Alifika nyumbani kwao bila kujua. Kidogo apapite. Alivuka barabara na kuifikia nyumba yao. Aliangaza huku na huko hakuona mtu. Alisukuma mlango na kuingaia ndani.
“Nilikuwa nakusubiri. We yaani tokea saa nane ndio unarudi muda huu! Unajua nakutegemea wewe tu, siwezi kutembea na miguu yangu hii mibovu!” Mama Tabu alisema huku akimwangalia Tabu kwa macho yaliyojaa lawama.
“Kwanza shikamoo mama.” Tabu alisema huku akimsogelea mama yake jikoni.
“Marahaba umechelewa wapi? Unieleze kwanza!” mama Tabu alihoji huku akiendelea kukaangaa maandazi yaliyokuwa jikoni. Tabu alimeza funda la mate na kumuomba mama yake amtazame aone jinsi alivyochafuka. Alimweleza jinsi alivyopwewa adhabu kwa sababu ya kuchelewa shule.
“Wewe Tabu kama unaona mambo yamekuwa magumu bora uache tu hiyo shule maana huko ni kuteseka tu. Nakuonea huruma sana mwanangu.’
“Hapana mama nitakomaa tu.”
“Sasa wee utaendelea kuumia kila siku kisa hali tuliyonayo?’
“Nitajua cha kufanya mamangu.” Tabu alisema huku akichukua andazi na kuling’ata.
“Elimu hiyo ya mahangaiko haitakusaidia chochote unapoteza muda tu.” Mama Tabu aliongea huku akiyaweka maandazi yake ndani ya ndoo.
“Usiseme hivyo mama, maana huwezijua ya kesho.”
“Utajua mwenyewe. Fua hizo nguo zako, mimi napika chai sawa?” Mama Tabu aliongea huku akichochea kuni jikoni.
Saa mbili kamili chai ilikuwa tayari jamvini, Tabu na mamaye walikunywa bila kuzungumza mpaka walipomaliza. Mama Tabu alikwenda kuoga. Tabu naye alikwenda chumbani kwake kujisomea.
Alipofika chumbani, Tabu alichukua kitabu chake cha kidato cha pili na kuja nacho sebuleni. Alisogeza taa karibu kabisa na kuketi. Dakika kumi tu zilipita, kisha, puu! Puu! Puu! Mlipuko wa taa ulisikika. Tabu aliangalia akajaribu kupandisha utambi lakini taa ilizidi kulipuka na mwishowe ikazimika. Giza totoro lilitawala. Tabu alipapasa huku na huko mara agongane na viti mara sufuria kidogo aingie mekoni. Alikishikilia vyema kitabu chake, akashika ukuta na kuanza kuupapasa huku akitembea kama kipofu. Aliufikia mlango na kuufungua. Anga lilikuwa lenye mwanga hafifu lenye mawingu ya hapa na pale. Nyota na mbalamwezi vilisaidia kuing’arisha dunia. Tabu alikaa kwenye kizingiti cha udongo. Ghafla mbalamwezi ilipotea na kuingia mawinguni. Tabu aliamua kunyanyuka na kwenda kulala.
Saa kumi na moja alfajiri Tabu alishitushwa na sauti ya adhana. Aliamka na kuketi. Alitumbua macho yake kwenye lile giza, hatimaye akanyanyuka na kuelekea bafuni. Aioga harakaharaka, akaanua nguo alizozilaza jana kweye kamba na kuingia nazo chumbani. Alipaka mafuta kisha akavaa harakaharaka na kutoka sebuleni. Aliusogelea mlango wa chumba cha mamayake na kuita;
“Mama, mama…?”
“Bee!” Mama Tabu aliitikia huku akijinyosha.
“Shikamoo. Ndoo ipi nichukue?”
“Marahaba! Chukua yenye mandazi, hiyo yenye keki iache nitauzia hapahapa nje. Halafu chenchi pia ipo hapohapo kwenye ndoo ya keki.”
“Sawa.”
Saa kumi na mbili kamili Tabu alikuwa stendi ya Maramba. Kazi yake aliipenda hivyo hakupata tabu. “Mandazi, mandazi! Ya motomoto! Matamu kama asali ya Zanzibar. Ya leoleo.”
“Oya sista nipe matatu mia tano hii hapa mia moja chukua kwa konda.”
“Na mimi nipe manne, hela hii hapa, changamka basi.”
“Usiondoke broo fasta nakupa just wait.”
“Huku nipe matatu changamka gari inasepa.”
Saa mbili kamili maandazi yalikuwa yamekwisha. Aliamua kusogea kwenye banda mojawapo la kupumzika ili aweze kuhesabu fedha zake.
“Aanh Tabu nakuona mshiko kama wote.”
“Wapi wewe zote ada tu.”
“Wewe acha zako mtoto unahela siku hizi.”
“Hela wapi bwana!”
“Acha uwongo taratibu tu hadi shule utaacha kama mie.” alisema Sadiki huku akimpa Tabu mkono.
“Heri uamue jambo moja Tabu mimi nahisi bishara itakutoa.”
“Mmmh biashara bila elimu, nyie wenywe mnavyobabaika kutoa chenchi yote shauri ya kuacha shule, bora mngeendelea tu kwa sababu mnapata maarifa.”
“Ni ukweli Tabu lakini mtu utawezaje kusoma huku tunafanya biashara?” alisema kijana mwingine aliyefuatana na Sadiki.
“Tutaenda kuongea nao hukohuko. Hata usijali tunahitaji elimu zaidi.” Tabu alisema huku akiziweka fedha kwenye ndoo ya mandazi.
Vijana wale na kuamua kuondoka wote kwa pamoja. Saa tatu kamili wote watatu walikuwa eneo la shule. Mlango wa darasa ulikuwa umefungwa. Tabu aliamua kugonga, “ngoo! ngoo! ngoo!” Kmya kilitawala lakini baada ya dakika mbili mlango ulifunguliwa. Mwalimu aliwangalia Tabu huku akimfuata, kiboko mkononi.
“Unachelewa halafu unasumbua sumbua.” mwalimu alisema huku amenyooshea Tabu kiboko, kisha akawageukia akina Sadiki, “Na nyie mmefuata nini hapa?”aliwatumbulia macho huku akiwafuata na kusema ile shule siyo ya machokoraa. Kama waliacha shule watajua wenyewe hawahitaji tena pale.
“Sisi tunataka kusoma. Tuna haki ya kusoma. Ni lazima tusome kwani elimu ni ufunguo wa maisha yetu. Tuliacha shule lakini sasa tumejitambua.” wote walipaza sauti kwa pamoja. Sauti zao zilifanya walimu na wanafunzi wengine wafike kwenye eneo la tukio. Wanafunzi walipiga kelele na wengine wakizaaga huku na huko.
“Msilete vurugu hapa. Hii ni tasisi, inahitaji utulivu.” Mwalimu alisema kwa sauti kubwa akijaribu kushindana na zogo la wanafunzi.
“Sisi pia ni wanafunzi tunahitaji kusoma.”
“Hebu jiangalieni. Je, mnafanania na watu wanaostahili kuwa hapa?” mwalimu aliwauliza huku akitazama nguo zao zilizo na viraka kila kona, sura zimewapauka nywele timutimu.
“Mwalimu jaribu kuangalia. Mpaka tumeamua kuja hapa tumeyatafakari yote hayo.” Sadiki alisema .
“Elimu na biashara wapi na wapi. Sitaruhusu mwanafunzi afanye biashara na kusoma.” mwalimu alisema huku akimtazama Tabu.
“Mwalimu uwe unatufikiria na sisi. Sio kwamba tunapenda kufanya biashara na kusoma ila inatulazimu.” Tabu aliongea huku akifuta machozi kwa upande wa nyuma wa kiganja chake.
“Nyamaza! Wewe ndio unazijua sana sheria za shule sasa enh? Ndio maana unatuletea vurugu hapa shuleni? Sasa utaenda kimoja kupumzika nyumbani.”
“Kwa kosa gani, Mwalimu?”
“Unajua kosa lako. Haitoshi kuwa unachelewa kila siku, sasa unaanza kutuletea watoto wa mitaani shueni?”
“Sisi sote ni watoto Mwalimu.”
Watoto wana haki ya kusoma. madhali wameamua kurudi basi tuwapokee ili waendelee kusoma. Hakuna haja ya kuwanyanyapaa. Kwanza Tabu njoo hapa. Wewe ni shujaa. Umeona umuhimu wa elimu ukawashawishi wenzio warudi.” Mwalimu Mkuu aliyekuwa amesikia zogo la wanafunzi akaja na kushuhudia malumbano ya Mwalimu na wale watoto aliongea huku ameshika Tabu mkono.
Tabu na wenzake walitabasamu. Shule nzima ilijawa na furaha kuwaona wenzao wameruhusiwa kurudi shuleni. Tabu walijiwekea mikakati ya kusoma kwa bidii na badaa ya masomo kuendelea na biashara ya kujikimu yeye na mama yake.

Gallery

Share the Post: