Tone la Damu

Art Type: Short story
Artist Name: Emmanuel Minja

“Hapana, lazima njia ipatikane, haiwezekani mimi tu miaka yote hii, kwani nimemtendea Mungu nini kibaya kiasi hicho? Wazazi nipoteze, ulimwengu unisulubu kwa masengenyo, nikonde, nilifeli kidato cha nne, muda wote huo jasho linimwagike kwa kuwa ati kilimo ndio mkombozi wangu? Ardhi yenyewe ipi Igunga hii kavu kama zulia la Ikulu?”
Kwa mbali nilisikia harufu ya kitu kinachoungua. Ilikuwa ni maharage niliyoyaacha jikoni kabla sijaja shamba kutafuta japo karanga zakuungia. Nilikiinua kiuno changu kama mjusi wa kondeni aonapo windo nono, haraka nikafyatuka hadi jikoni. Sikupepesa jicho, nilikikamata chungu nikakitupa chini paah! Kilitua pembeni mwa vifiga vilivyokosa afya. “Ah! Maharage yenyewe yaliyoungua mawili? Nilifikiri jungu zima!”
Nilimimina maji kutoka kwenye jagi nikakirudisha chungu mekoni, kisha nikaanza kuitafuta simu mfukoni. “Nimpigie nini? Rajab, Rajab ni jibu langu!” Katika mazungumzo yetu ya awali, nilijitahidi kumchunguza. “Huyu jamaa atakua na njia bora zaidi.” Simu haikuweko mfukoni.
Maharage yaliendelea kuchemka jikoni wakati nikiwa naandaa vikaranga vyangu. Mawazo yalihamia katika simu. “Nimeiacha wapi?” Mara ya mwisho nilipoitumia nilikuwa kwenye kichanja cha vyombo. “Huenda ndipo nilipoiacha na inawezekana Rajab ameshaujibu ujumbe wangu.” Ilinibidi kukiacha kigoda changu niifuate simu ili kujua kilichojiri. Niliikuta hapo nikamwelezea Rajab namna ninavyoteseka na shughuli za kijijini ambazo hazinipi faida yoyote zaidi ya kunidhoofisha.
Katika kipindi kifupi tangia wazazi wangu wafariki, uso wangu ulizidi kukondeana na mwili wangu ukisadifu umbile la mnazi. Baada ya dakika saba tu baada ya kufanya maongezi na Rajab, alinitumia ujumbe mfupi akinijulisha kuwa yupo tayari kunisaidia, tena atakuja kijijini kwa ajili ya safari yetu kuelekea Dar es salaam ambako tutaenda kufanya biashara.
“Mungu si Athumani. Waliotabiri anguko langu sasa yatawapwaya.” Nilijisemea nikasonga na kula ugali wangu kwa furaha sana mchana ule, sio kwa suprize ile ya Rajab!
Machweo matatu tokea siku ile, sikuwa naihisi baridi kali ya Igunga tena. Nilihisi niko Dar tayari. Rajab akiwa amekwisha wasili tulipanga namna tutakavyosafiri kuelekea Dar. Pamoja na picha za Jiji la Dar ambazo zilinitia morali ya safari, Rajab alinikosha zaidi pale aliponiambia mpango wa kusafiri na lori za mizigo kutokea nchi jirani. Aliniambia amechonga na washikaji alipokuwa anakuja Igunga wakamtonya kuwa kuna uwezekano wa kupata mteremko wa kutufikisha hadi Dar es salaam. Cha msingi kuset muda mzuri na mahali poa. Nilijihisi mwenye bahati kama malaika duniani. Pesa ya nauli imeokolewa, pesa yenyewe kichele.
Pandisha mikono, shusha, pandisha, shusha, pandisha shusha, wapi! Hakuna lori lililosimama. Taa zilitupita na upepo wa mwendo kasi ukizipangusa nyuso zetu. Nilikata tamaa, nilidhani labda haikuwa siku ama saa sahihi ya sisi kuondoka Igunga. Labda baadae au kesho. Nilisogea nyuma kidogo lakini Rajab hakukata tamaa. Yeye aliendelea kukaa kando ya barabara huku akiuangalia mkono wake kila mara kama mtu aliyeumizwa na kitu. Hakukatishwa tamaa na muda, alikuwa akiitizama saa yake na kila alipoweza aliyapungia malori mengine, japo kwa kubahatisha!
Giza lilizidi kuwa totoro. Mwanga mkali zaidi ulionekana kutokea upande wa barabara itokayo Geita kwenda Singida. Sikufahamu ulikua ni muda gani. Nilifikiria kumuuliza Rajab ambaye aliitazanma saa yake na kisha kusimama. Nilidhani safari ndo imeyeyuka kama barafu na kupepea kama karatasi. “Huyu hatasimama na muda umekwenda sana. Labda tujaribu siku nyingine.” Niliyaumba maneno hayo nikidhani ndio yatakayozaliwa kinywani mwa Rajab. Taa ziliposogea zaidi, Rajab naye alisogea barabarani zaidi. Wakati huu alitembea hadi katikati ya barabara. “Ha! Anaakili kweli huyu? Anajifanyia nini pale?” Nilijikuta nimeshafika barabarani na kumkwapua Rajab alipokua amejiezeka, hadi pembeni ya barabara. Alinigeukia bila kusema lolote, akaukwida mkono wangu na kunichoropoka. Alirudi barabarani, akainyoosha mikono yake yote miwili. Alichoreka kama mtu anayetaka msaada wa haraka, ama mimi mimemvamia au kuna hatari mbeleni. Nilihisi kuchanganyikiwa na kutojua la kufanya. Macho yakiwa yanaona mazigazi, nilihisi mikono yake ikinisukuma pembeni huku akisema;
“Huyu atasimama.”
“Wewe, unafanya nini?” nilijikuta nikimuliza kwa sauti ya kukaripia iliyochanganyika na uwoga.
“Tulia, gemu nililocheza lazima asimame.” Alipomaliza kusema hayo, Grrrrrr! Kelele za breki zilizochoka zinafungwa pembeni yetu ukachomoza uso mwembaba wenye gadhabu kutoka ndani ya lori lile, uliobebwa na mwili nyorodofu ukiwa umetilia kofia kama ya wacheza gofu.
“Kuna shida gani?” dereva aliongea kwa sauti ya dharau huku akimkazia macho Rajab na kunipa mimi kisogo. Kwa kujaribu kuondoa hali ya Rajab kupigwa kofi, nilimjibu dereva yule, japo kwa kutetema sauti. Rajab alidakia na kuanza kumwelezea dereva yule mambo ya kubuni yanayotusibu.
Kwa takribani dakika mbili, ulumbi wa Rajab ulifanikiwa kupata ruhusa ya dereva yule. Alituambia anakwenda kupumzika kwenye kontena, hivyo Rajab achukue usukani hadi dodoma ambapo tutamwamsha aendelee na safari yake. Bila kupoteza muda tulirukia kwenye lori, uso wangu ukionesha tabasamu mwanana. Rajab aliitupia leseni yake kwenye dashi ya dereva huku mkono wake mmoja ukianza kuamsha gari.
Safari ilipambwa na masimulizi ya ushujaa, hasa nikimsifu Rajab kwa uhodari wake na namna alivyoweza kumiliki matukio hadi kuweza kupata nafasi ya kuanza safari. Tukiwa njiani Rajab alishauri tuingie kwenye mkahawa mmoja anaoujua takapate kahawa. Nilitoa wazo la kutumia chupa yangu ya chai kumhifadhia mfadhili wetu, japo kumfanyia ukarimu, nikiwaza kama angelijisikiaje kuamshwa na kupatiwa kahawa. Tukiwa tumepata vikombe kadhaa vya kahawa tulirudi lorini huku tukiwa tunazungumzia wingi wa watu tuliowakuta ndani ya mkahawa ule, hasa wakati kama ule. Rajab aliniambia ni mkahawa uliopendwa zaidi na madereva wa malori wapitao njia ya Shelui kabla ya kufika Singida mjini. Ama kweli mkahawa ule ulishiba wateja.
“Dodoma haitaweza kuwa mwisho wa safari yetu. Itabidi tumshawishi mjamaa zaidi tuteremke nae hadi Dar, au unaonaje?”
“Yeah! Unaonaje tukamshawishi wakati tunampa kahawa, ataona sisi ni watu wakarimu.” nilimjibu Rajab huku uso wangu ukiangalia kioo cha mbele kwa macho yenye tafakuri. Na jinsi ulivyo fundi wa maneno, ukimkalia freshi mbona hakishindikani kitu? Nakuaminia Rajab.”
Miguu na mikono ya Rajab vilishirikiana vilivyo kuliburuza lori lile mpaka Dodoma. Si asubuhi bado, ilikua ni muda sahihi wa kumwamsha mfadhili wetu na kuanza mazungumzo yetu. “Akinywa kahawa tutapiga nae stori za hapa na pale na kuchukua nafasi ya kumshawishi bonus ya safari. Hakuna namna atachomoka.” Rajab akishughulika na kupooza injini, niliteremka na kwenda nyuma ya kontena kumwamsha mfadhili wa safari yetu. Kwa bashasha niliufungua mlango wa kontena.
Viroba kibao. Magunia ama matenga ya matunda na viungo ndio picha iliyochoreka kichwani kwangu nitapofungua kontena. Nilistaajabu kuona viroba kadhaa! Ina maana mzigo mzima wa huyu jamaa ndo hivi vijiroba! Kupanda ndani ya kontena ili nimwamshe, vidole vinagusa unyevu wa ajabu kidogo. Unyevu unatelezateleza, ukiunusa una harufu mbaya. Sikuweza kuuona vyema kwa kuwa ndo kwanza alfajiri ilikua inakaribia. Kuwasha tochi ya simu yangu, vidole vyangu vilienea damu. Nimejikata na nini? Kumulika zaidi kwenye kontena, naona michirizi ya damu ikiongezeka kadri inavyozidi kusogea mbele. Ameuliwa? Mawazo yaliniruka. Hatukusikia mkwaruzano wowote, ama tulivyokua mkahawani? Na mwili wake uko wapi? Nilihisi nywele kusisimka kwa woga ulioniingia. Kichwa kikawa cha baridi, ngozi ikafa ganzi na macho yakasafiri na akili. Niliganda kwa sekunde kadhaa. Nikaruka kutoka katika kontena lile kisha kumfuata Rajab ambaye alionekana kuielewa taharuki yangu bila hata kujieleza. “Amekufa!” Ndo neno pekee nililoweza kutamka mbele ya Rajab.
Aliteremka kama mtu aliyejiamini zaidi na kuelekea eneo la tukio, japo hatua zake hazikuonekana kuwa za kijasiri. Ubongo wake ulielekea kutawaliwa na sintofahamu iliyooneshwa na macho yake. Alifungua kontena huku nikimfuata. Alipoingia ndani alimulika kote. Damu ile ilipoanzia ulionekana mwili tofauti kidogo. Ni mwili wenye ujazo kidogo, kichwa kipara, na mfupi kiasi. Si mwili wa mtu aliyetufadhili hapo awali. “Ni nani huyu?” nilijiuliza kwa sauti iliyomfikia hadi Rajab.
Rajab akionekana kuzidiwa na mawazo, aliniuliza akiwa ananiangalia kwa umakini, “Kwani kontena lilikua limefunguliwa?”
“Hapana!”
Alirudisha macho yake kwenye mwili ule baada ya kupokea jibu langu. “Ni wezi. Angalia hata mzigo wenyewe wameiba. Haiwezekani kontena libebe mzigo kama huu. Hapa hata kirikuu si kingebeba! Waliiba tulipokua mkahawani, walimpoteza mjamaa labda alileta ubishi alafu wakamweka huyu mshikaji ili kututisha, au kutuuzia kesi”. Nilijaribu kuyatetea mawazo yangu, japo nipate sababu ya kuamini. Kisha uso wa Rajab ulibadilika. Alionekana kuingiwa na hofu;
“Ramadhani?” hakuniita Rama tena safari hii. “Tuondoe kesi hii hapa. Pakia kwenye gari tutafute sehemu ya kupoteza ushahidi. Inabidi tutokomee porini, tutajadili zaidi mbele ya safari.”
Sikua na muda wa kuwaza, kilichofuata ni kuingia hima na kutimua ndani ya lori. Kimya kilitawala katika siti zile mbili. Rajab akitazama mbele kwa tahadhari kubwa. Akili yake ikionekana kuwa mbali. Nikimtazama kwa kuibiaibia nikihisi tumbo kuchanganya kwa uwoga. Tulisonga mpaka kajua kalipoanza kuchomoza bila kupata pori la kusitiri matatizo yetu. Nilishindwa kumuuliza wapi haswa? Muda gani? Kwani yeye ndiye aliijua njia zaidi. Nilipoona hali ya ndani mle inazidi kuwa ngumu. Ukimya uliopitiliza na hofu binafsi zinazoonekana kwenye nyuso zetu, niliamua kuuliza tunafanyaje, kama mpango mbadala, angalau kuipa uhai safari yetu. Mawazo yetu yalikithiri kwenye kadhia iliyotukabili ikatusahaulisha kusahau madhumuni mahususi ya safari yetu.
“Lakini nani aliyeyafanya yale?”
“Haitasaidia kwa sasa Rama!” sauti ya Rajab ilitoka ikiwa imegubikwa na hasira na majuto. Hapana, nilitaka kutamka jambo lakini nikaona bora kukaa kimya.
Mishale ya saa ya Rajab ilisoma saa mbili asubuhi. Nikizidi kumwangalia, nilimuona akikaza macho yake mbele ya kioo kwa umakini Mkubwa. Mwendo ulianza kupungua hadi alipoegesha kando ya barabara.
“Kuna tatizo?”
“Naenda kuchimba dawa.” alinijibu kwa kifupi Rajab huku akishuka haraka kwenye vindato vya mlango wa lori lile.
“Usiende mbali.” nilimsisitizia kuashiria uwoga niliokuwa nao wa kuachwa peke yangu.
Kuangalia mbele ya kioo cha lori vizuri, namuona polisi wa usalama barabarani kwa mbali amegeukia upande wetu. Moyo ulidunda kama unataka kutoka. “Hatajua kitu. Hajamwona Rajab akishuka. Nitatulia humuhumu ndani.” nilifanya mazungumzo ya peke yangu ndani ya lori kujipa moyo huku polisi akilisogelea lori.
Zilipita dakika takribani tano bila Rajab kurudi. “Dawa gani anachimba? Wapi? Hii hatari ikija mimi nafanyaje?” nilijiuliza maswali niliyoshindwa kupata hata robo ya mwafaka. “Nashuka, isije ikawa Rajab anafanya jambo la hatari huko nyuma bila kujua hatari inayokuja.”
“Kijana?” sauti kali yenye msimamo thabiti ilitoka kutoka kwa mama yule aliyejishoza kwenye sare za polisi. Sauti hiyo ilinidaka punde nilipotua chini. Niligwaya kidogo kisha nikajikaza bila kumjibu chochote. “Mnafanya mchezo gani? Mwenzako yuko wapi?”
“Mwenzangu?” nilijidai kutomuelewa.
“Hujaelewa nini hapo?”
“Hapana, hatufanyi mchezo wowote.”
“Dakika kumi sasa tangia azamie huko porini, hajarudi na wewe unajishusha uende wapi? Mnanichezea ee! Hapa mmegonga mwamba.” Maneno yake yalivuruga kila utumbo ndani ya mwili wangu, nilihisi ardhi angalau inimeze na kunitapikia Igunga.
“Mtaka cha uvunguni sharti ainame, na kama kuinama kwenyewe ndo huku, vya uvunguni vibaki hukohuko.” Niliwaza. Nikiwa katika mparaganyiko huo, polisi alinisomea mashitaka ya kuendesha mwendo kasi katika safari yetu. Alinionesha na picha ambazo hata sikumbuki zilifananaje akidai ndio ushahidi wa kosa letu. Akiyaongea yote hayo, nilifanikiwa kubaki na macho yangu tu, akili yangu ilimuwaza Rajab, “Iweje ayaone yote haya na hata asinijuze? Ina maana ni kweli amenikimbia ama akiwa njiani kurudi alishtukia kinachoendelea akajibanza? Na akijibanza yeye, mimi nisiye na mbele wala nyuma nitaeleza nini.?”
“Naomba leseni zenu.” aliamrisha polisi.
“Mimi siendeshi gari.” Nikakumbuka Rajab alipoitupia leseni yake, nikamwambia nitampa ya aliyekua akiendesha. Alipomaliza kuiangalia, akaniuliza mwenzangu yuko wapi. Kwa ushapu nikajibu, anaumwa tumbo.
Macho yake yalipunguza ukali kiasi, nikashusha pumzi taratibu ili kujiweka sawa. Aliweka sawa mashine yake ya risiti, akaanza kuandika faini yetu. Alianza safari ya kulikagua lori.
“Akijichanganya nasepa!”
Alipofika kwenye kona ya nyuma, aligeuza uso wake kunitazama ghafla kabla sijapata mwanya wa kutimua mbio.
“Kuna nini humu ndani?”
“Wapi?”
“Humo. Hunisikii au, njoo hapa!”
Nilianza kuburuta miguu yangu kumfuata huku nikitafuta uongo wowote ulio karibu. “Hii ni nini?”
“Damu!” nilimjibu nikiujenga uso wa mshangao na kuzuga kama sijui kilichopo ndani. Nnilimdanganya kuwa nimepewa lifti, sikuwa na ufahamu wowote kuhusu kilichopo ndani ya kontena. Alinitazama kiyakinifu kisha akaniamuru nifungue kontena lile. Uvundo wa kuzimu gani?!
Jua lilivyozidi kupambazuka ndivyo magari mengi ya polisi yalivyofika eneo la tukio. Hakukuwa na Rajab, bali mimi na maisha yangu tu. “Ninavielezeaje viroba vile vya madawa ya kulevya na maiti nisiyofahamu hata ncha ya historia yake? Yamenikuta haswa!” niliwaza.
Pingu mkononi, niliwasilishwa kituo cha polisi Gairo. Ilikua ni aidha uhuru wa maisha yangu ama kufa masikini. Nani atachagua kupoteza uhuru wa kuishi. Niliamua kutoa kila ushirikiano utakaohitajika kwa polisi. Nilielezea kila jambo na namna lilivyotokea. Mdada aliyevalia suti nyeusi aliingia kwenye chumba maalum pamoja nami. Alifanya upelelezi wa kesi kwa maswali kadhaa kisha akanipa ruhusa ya kusema ambayo ningependa ayafahamu.
Sikuyaamini masikio yangu kwa ripoti ya upelelezi, Rajab, rafiki yangu tangia shule ya sekondari aliamua kuniwekea mtego mimi. Tena jirani yake. Ukistaajabu ya Musa utayaona ya Firauni! Kwa uchu wa fedha za magendo, Rajab alishawishika kuutumia umasikini wangu ili aweze kujiongezea mali. Sasa nilielewa sababu ya kuangalia saa yake kila sekunde, hata kujifanyisha kwake alipoona taa za lori lile. Baada ya wiki nikiwa nimerudi kijijini, mipango ya kilimo ilishamiri. Sikuona tena njia nyepesi ya fanikio; hata moja.
Nilihuzunika nilipoitazama picha ya Rajab. Masikini alishapoteza dira ya maisha. Ataozea jela pamoja na wenzake. Ila hofu bado inatanda kichwani mwangu, “Ni nani aliyekuwa dereva wa lori hapo awali? Je, alitiwa nguvuni ama ndio mzazi wa cheni mpya ya biashara ile?” Nahuzunika siwezi kuhakiki hilo kwa kuwa sikupata kumtia machoni. “Jamii ipo salama?”

Gallery

Share the Post: