Safari ya Matumaini

Art Type: Short story
Artist Name: Ayubu Mashaka

Juma aliamshwa usingizini na sauti ya zogo lililosikika kutoka nje. Alijivuta taratibu kutoka kitandani akapepesa macho na kutazama juu ya mlango wa chumba chake. Alitungua nguo alizozining’iniza mlangoni akazivaa. Alifungua mlango akatoka nje. Nje alikutana umati wa wapangaji wenzake.
“Kwani kumebomoka saa ngapi?” sauti ya mama mmoja ilisikika akiliuliza.
“Toka jana, saa mbili usiku.”
“Sasa toka jana mnajisaidia wapi?”
“Tulijikaza ila tumekubaliana tutatafuta na kuvifunga viroba kwenye uchochoro huo huko nyuma.” alijibu kijana mmoja akinyoosha kidole kuelekea nyuma ya chumba kilichopo karibu na choo hicho kilichobomoka.
Juma aliwasikiliza wale watu waliozingira kile choo pekee kilichotegemewa na familia zote katika nyumba hiyo ya kupanga. Aliubana mkojo akiwaza atajisaidia wapi, ataoga wapi na vipi ikija ile haja kubwa atafanya nini. Aliangazaanganza macho kuelekea kwenye kichaka kilichoko karibu, akatoka haraka bila kusalimia. Aliporudi alikuta ugomvi na tafrani kubwa.
“Kuna nini? Kuna nini jamani?” Juma aliuliza huku akipandishapandisha msuli aliokuwa ameuvaa. Juma alijipenyezapenyeza mpaka akafika katikati ya umati ule. “Tulieni, tulieni jamani.” alijaribu kutuliza zogo lile bila mafanikio.
“Acheni, acheni jamani. Punguzeni jazba.” Juma alizidi kusihi huku akiwatazama kwa awamu wanawake waliokuwa wakibwatizana na kijana mmoja mpangani mwenzao.
“Mama Tunu nini tatizo?” aliuliza Juma.
“Huyu Chitanda mpuuzi sana!” alijibu Mama Tunu huku akijivuta na kumshikilia vizuri Chitanda kwa kumvuta shati.
“Kafanyaje sasa?”
“Si kajisaidia nyuma ya choo! Kweli mtu mzima kama huyu anawezaje kufanya mambo ya hovyo kama haya?”
“Ah, hebu muachilie kwanza tuyaongee kiutu uzima.”
“Haachiwi mtu hapa mpaka azoe!” Mama Tunu alijibu.
“Tukimuacha atazoea.” Mpanganji mwingine alidakia.
“Muachieni tuyaonge jamani. Sasa, mlivombana hivyo ataongeaje?” Juma alisema huku akiwakaribia akina mama wale waliokuwa wamemkamata Chitanda akaendelea kuwasihi wamuachilie.
Mama Tunu na wenzake walimuachilia Chitanda huku wakimkodolea macho. Chitanda alijitandaza pale chini kama aliyekufa, nguvu zimemuisha. Juma alimshika begani akalipigapiga huku akisema, “Kijana mbona unafanya mambo ya aibunamna hii?”
Chitanda alibaki amenyamaza tu. Hakuwa na la kusema jinsi aibu zilivyomshika. Juma hakuona haja ya kuendeleza kuaibishana. Aliwaomba watu waondoke ili aweze kuongea naye vizuri.
“Haiwezekani! Huyu lazima tumfundishe adabu.” alisema Mama Tunu.
“Jamani tuwe wastaarabu. Mimi nitaiongea naye.” Juma aliongea kwa msisitizo. Baadhi ya watu walianza kutawanyikia. Hatimaye Juma na Chitanda walibaki peke yao wakiwa wanatazamana. Juma alimsihi Chitanda azoe kinyesi kile na akamsimamia. Alipomaliza, Juma aliingia chumbani kwake mawazo yakiwa yametawala katika ubongo wake. Alichukua simu na kumpigia mjomba wake;
“Mjomba kesho nataka kuja huko.”
Juma alikata simu. Alikuwa ameketi juu ya kitanda. Mawazo mengi yalimuandama. Aliyawazia sana maisha yake akahisi kuvurugikiwa kila wazo jipya lilipopandana na lililokuwepo.
“Nimekuwa kama kuti kavu ninasubiri kudondoka. Kodi ni shida, chakula ni shida, kila kitu kwangu mtihani. Eeenh Mungu nisaidie. Ndugu na jamaaa wamenitenga. Hakuna msaada. Naona kama narudi nyuma. Nimeanguka nashindwa kunyanyuka!” Juma alichungulia dirishani huku mawazo yakimsakama. Alilishika tumbo lake lililokuwa limeanza kunguruma. Alipapasa mfuko wake wa shati. Alijisachi kwenye mfuko wa suruali. Hakuwa na kitu chochote….
Juma aliketi kwenye kitanda chake cha kamba huku akilishika tumbo lake. Alinyanyua miguu yake na kuiweka kitandani. Alijiegemeza huku akiwaza. Hatimaye usingizi ulimchukua. Alishitishwa na kuti lililopiga juu ya paa lake la nyumba, akazinduka, “Mmmmh nini hiki tena?” aliamka na kuzunguka nyuma na kukuta kuti likining’inia juu ya paa. Juma alitazama na kutikisa kichwa kisha akarudi tena chumbani kwake.
Siku iliyofuata, Juma aliikumbuka ahadi ya kwenda kwa mjomba wake. Alitoka nje, akafunga mlango wake na komeo kisha akaanza kupiga hatua kuelekea upande wa magharibi. Alishika njia iliyopo mkono wake wa kulia. Alitembea kupitia kwenye eneo lenye uoto wa asili, mashamba ya chai, migomba na mihogo. Aliangalia eneo lile lenye milima na mabonde yaliyopiga kijana kilichokoza ambayo yalivutia mboni za macho yake na kuusifia uumbaji wa Mungu Mwenyezi. Juma alitembea akibembelezwa na upepo mwanana, hadi kwa muda aliisahau njaa aliyolala na kuamka nayo. Ghafla upepo ulianza kuvuma kwa nguvu, nuru ikapotea. Manyunyu ya mvua yalitapakaa na kuivaa anga. Juma alijibanza kwenye shina la migomba. Mvua ilipokata aliendelea na safari yake.
Saa tatu kamili Juma alikuwa amefika Gulilo, kijiji kinachopakana na kijiji chao. Barabara ilikuwa imeharibiwa na mvua, hivyo magari yalikwama na matope yalikuwa yametapakaa kila mahali, hivyo Juma alinyanyua suruali ya jinsi huku ndala zake ziking’ang’ania matopeni. Aliangaza macho yake huku na huko. Alikutana na njia panda akaamua kuelekea barabara iliyopo mkono wakulia kwake. Alikaza mwendo wake na kuanza kuliacha pori, Mbele kidogo alianza kuona makazi ya watu. Mbele kidogo aliwaona watu wanakusanya marundo ya mihogo. Wanunuzi walikuwa wamezagaa wakitaka huduma;
“Anko nipe mihogo fungu mbili.” alisema mwanamke mmoja huku akifungua mfuko; na mwingine akaingilia;
“Jamani niwekee na mimi ona hiyo inaisha jamani we kaka.” Na mwingine;
“Fasta kaka, nitakwenda kwingine mimi. Au unaringa kwa sababu unajua tunaohitaji mihogo tuko wengi?”
“Oya, binti tulia nakuwekea mihogo. Hapa imekwisha ila nitasafiri kuifuata shamba usiku huu. Utaikuta asubuhi.”
“Jamani kumbe maisha huku ndivyo yalivyo? Hivi kijijini kule akina mjomba wanakaa na mihogo mpaka inaharibika kumbe watu huku wanaifanya fursa? Haki ya Mungu usilolijua ni usiku wa kiza.” Juma aliwaza huku akipepesa macho. Alizubaa kwa muda, wimbi la mawazo likimsonga lakini aliendelea na safari yake. Ilipofika saa nne na nusu, alifika kijijini Mkwicha. Hapo palikuwa na stendi ndogo. Mwili mzima ulimuuma kutokana na uchovu aliokuwa nao. Alitembea kwa kujivuta kama chatu. Alifika karibu na bao la kukalia, alijipweteka akashika tama huku akitupatupa macho yake huku na huko.
“Broo! Maji buku, vitumbua vitano jero. Saa buku nne. Chagua upendacho bei tunaongea.” Jabiri aliongea huku ametupia miwani yake nyeusi huku akitingisha tingisha kameza kidogo alichokuwa amekibeba.
Juma alimwangalia yule kijana. Kwa umri alikuwa na miaka kumi na tatu kwa kukadiria, mnene wa sura, macho yake madogo yalimfanya aonekanne kama anamtumbulia macho. “Mimi ni mtu wa namna gani?” Juma aliwaza. “Kwa nini nisifanye kitu ambacho kitabadili haya maisha ya utumwa ninayoishi mjini? Yaani rasilimali zipo, kwa nini nipate tabu namna hii?” alijiapisa mwenyewe kuwa atajizatiti kupambana na atashinda. “Nitaweza kwa sababu majaribu ndio ngazi. Nitamweleza mjomba matatizo yangu yote. Naamini atanisaidia hata kwa mawazo. Ni mwaka wa kufanya mabadiliko huu! Kwanini niteseke?”

Gallery

Share the Post: