Mifupa Hai
Mawazo yalikuwa yakikinzana kichwani kwa Shida. Ilionekana dhahiri. Aliwaza na kuwazua lakini hakulipata jibu kamili. Akaduwaa kwa muda kisha akajisemea, “Nitaenda naye kwa kuwa yeye pia ni binadamu. Bila shaka atanielewa tu.”
Shida akiwa amekaa chini ya mti uliokuwa umepandwa kando ya kibanda chao. Muda mfupi baadaye alitoka pale kivulini na kuingia ndani huku mawazo yakiwa bado yanauchezesha ubungo wake. Moja kwa moja akaenda hadi chumbani kwa mama yake. Alimkuta akitetemeka. Mwili wote ulikuwa umelowa jasho na mapigo ya moyo wake yalikuwa yakienda kwa kasi ya foji.
Shida alipomtazama mama yake chozi lilimdondoka mithili ya teja atoavyo udenda. Taratibu akausogeza mkono wake hadi kifuani kwa mama yake na kusema, “Usijali mama. Utapona tu.”
Asante mwanangu duniani ni raha na taabu.” Mama Shida alisema huku meno yake yakiumanaumana. “Nenda kwa Bwana Tozi mwanangu. Mwambie atukopeshe hela ili niende hospitali kupata dawa.”
“Sawa mama wacha niende saa hizi ili niwahi kurudi.” Shida aliongea na kuchukua khanga yake tayari kwa kuondoka.
Shida alikuwa ameumbwa akaumbika! Macho yake remburembu yalimfanya kila kijana aliyekutana naye avunje ghala yake ya ukimya na kuropoka chochote alichojisikia kuropoka juu yake. Wakati mwingine hata wazee wenye heshima zao walijikuta wakijikwaa kila walipomwona Shida akizichanganya hasi na chanya zake.
Shida alihesabu miamba kwa muda kisha akafika kwa bwana Tozi. Alijisogeza taratibu hadi mlangoni. Akaunyoosha mkono wake ili agonge mlango lakini akasita. Akanyoosha tena akasita. “Lakini acha nijiamini.” Shida alijisemea moyoni mwake.
“Ngo! ngo! ngo! ngo!” Shida aligonga mlango kwa wasiwasi. Sauti nzito ilisikika kutoka ndani ikisema,
“Ingia kupo wazi.”
Shida akausukuma mlango kisha akaingia ndani.
“Karibu uketi hapa.” Bwana Tozi aliongea huku akimwonyesha kochi lililokuwa karibu na Televisheni.
“Asante.” Shida alipita na kukaa.
Utulivu ulitawala kidogo wakati Shida alitafakari namna ya kuianza mada iliyomleta. Alijaribu kuiba jicho kwa Bwana Tozi, macho yao yakagongana. Wote wawili wakaangalia chini. Shida alikuna kichwa kisha akaanza kumweleza Bwana Tozi shida iliyomleta,
“Samahani kwa usumbufu Bwana Tozi.” Shida alisema kwa unyenyekevu.
“Bila samahani Shida.”
“Mama yangu ni mgonjwa sana. Hivi ninavyoongea nimemwacha kitandani akiwa hana mtu yeyote wa kumwangalia ila ameniagiza kwako nikuombe utukopeshe kiasi cha shilingi elfu ishirini tu halafu baada ya kuuza mazao yetu tutakulipa pesa yako.” Shida alisema huku akionesha hali ya uhitaji.
“Ni kweli pesa ipo lakini huwa naitoa kwa watu wenye vigezo maalumu; kwanza kama una kitu chochote cha kuweka rehani ambacho kinaendana na thamani ya mkopo unaohitaji.” Bwana Tozi aliongea huku akitikisatikisa miguu yake. “Lakini hujachelewa bado. Kama na wewe unataka kupata msaada wangu, ni lazima uwe na msaada kwangu maana mkono mtupu haulambwi.” Bwana Tozi aliongea huku akimsogelea Shida. Taratibu akautoa mkono wake na kuelekeza kwenye paja la Shida lililokuwa limeshiba sawasawa.
Shida aliushika mkono ule na kuutupa mbali huku akiwa ameikunja sura yake mithili ya jongoo aliyemsikia mwenzake akiwika.
“Toka hapa! Jitu zima hovyo! Huna hata aibu? Yaani shida zangu ndo zinifanye mimi niuze utu wangu?” Shida alibwabwaja kwa hasira huku akiwa ameshika mlango tayari kwa kuondoka.
Bwana Tozi akabaki kaduwaa bila kujua nini cha kufanya. Shida akaufungua mlango akaanza safari ya kurejea nyumbani huku mikono yake akiwa ameiweka kichwani mithili ya mtu aliyeshikilia furushi. Hatua zake zilikuwa kubwa zaidi ya zile za mwanzo. Kila alipowaza juu ya mama yake ndipo mwendo wake ulipozidi kuongezeka. Akakata kona kadhaa wa kadhaa kisha akafika nyumbani na kuingia moja kwa moja hadi chumbani alikomwacha mama yake akaketi kitandani.
“Shikamoo Mama” Shida alimsalimia mama yake kana kwamba ndio kwanza wanaonana siku ile. Akiwa bado ameketi kwenye kitanda alichokuwa amelala mama yake, Mama Shida alimuliza kwa sauti chini ilikuwa imejaa mikwaruzo, kama ni kwema huko alikumtuma au la.
“Siyo kwema mama.”
“Kwa nini mwanangu?” Mama Shida alihoji.
“Bwana Tozi amekataa kutukopesha japo amedai pesa anayo, ila yeye anadai kuwa hatuna vigezo vya kuweza kupata mkopo kutoka kwake.
“Kwa nini?” Mama Shida aliuliza.
“Kwa kuwa hatuna kitu chochote ambacho tungeweka rehani chenye kuendana na thamani ya mkopo tuonauhitaji. Hata hivyo nimejaribu kumwambia kuwa tutamlipa baada ya kuuza mahindi yetu lakini hakuonesha dalili yoyote ya kunielewa, kwa hiyo nimerudi kama nilivyoenda.” Shida alimjibu mama yake huku akiwa ameshika tamaa.
“Kwa hiyo tutafanyaje mwanangu maana naona hali yangu inazidi kwenda kombo?” Mama Shida aliuliza kwa sauti za chini kana kwamba anajihoji yeye mwenyewe.
“Mimi naona tuuze mahindi ili ukapate fedha ya kununulia dawa mama.”
“Sawa lakini huoni kuwa tutapata upungufu wa chakula maana mahindi yenyewe ndo hayo tu mwanangu?” Mama Shida alihoji. Baada ya kushawishiwa na mwanaye akipiga haidhuru akaridhia ili mradi upone kwanza. “Basi chukua zile gunia mbili ukaamuuzie bwana Tozi japo bei yake ni duni sana.”
“Sawa mama.” Shida alikubali na kuelekea nje.
“Yaani niende tena kwa Bwana Tozi? Hata siwezi kwenda kwanza bei yake ni kinywaji sana. Yaani gunia analonunua kwetu kwa shilingi elfu 20 yeye anaenda sokoni kuliuza kwa shilingi 40,000/=. Sasa kwa nini nisiende mwenywe sokoni? Ah! Nitaenda tu sokoni lakini vipi usafiri je?” Shida alijiuliza,akajijibu mwenyewe na kujiuliza tena.
Kwa kuyafuata mawazo yake, Shida aliamua kuazima torori la jirani yake, John, kisha akapakia mzigo, akamuaga mama yake ya kuwa anaenda kwa Bwana Tozi. Taratibu akaanza safari kuelekea sokoni. Akiwa amekaribia kuingia sauti za kila aina zilipenyeza kwenye masikio yake.
Mara ‘mteja mfalme’, ‘mpende mwanao’, ‘bei karibu na bure’, ‘chochote mia tatu’. Shida alifika akakokota torori lake hadi kwenye soko la mahindi na kulipaki. Aliuegemeza mkono wake mmoja kwenye torori lile. Muda si mrefu akaja mzee aliyekuwa amevaa shati la mikono mirefu na kizibao, chini alivaa suruali ya kaki na viatu vya mchongoko tumbo lake lilikuwa lipo mbele mithili ya mama mjamzito.
“Vipi dada,” Mzee aliuliza.
“Safi karibu.” Shida alijibu huku akikenua meno kuvutia biashara.
“Gunia moja la mahindi shilingi ngapi?” yule baba aliuliza.
“Elfu 40.” Shida alijibu.
“Basi naomba upime yote.”
“Sawa Shida alishusha mzigo na kuanza kupima. Baada ya kupima na kulipwa alitoka kasi. Alihisi kama kipofu aliyeona mwanga. Alipepesa macho yake huku na huku akijaribu kuchunguza kama kuna mtu yeyote anamtazama. Akavuta upande mmoja wa kanga yake na kuweka zile hela kisha akafunga fundo kuining’iniza ile khanga mgongoni mwake.
Matatizo alikuwa amejibaza pembeni akiwa anausoma mchezo mzima, hususani lile fundo lililokuwa ilimofungiwa ile hela. Taratibu akaanza kumyatia Shida wakati akiwa anajipenyeza katika katika ya umati wa watu pale sokoni huku anasukuma toroli. Matatizo akachukua wembe akakata lile fundo, akakwapua hela zote Bila shida kujua kisha akatoweka.
Safari hii Shida alirudi nyumbani huku akiwa ameyaachia meno yote nje. Alikimbiza torori kwa John ili awahi kumpeleka mama yake hospitali. Ilikuwa yapata saa nane mchana alipofika nyumbani kwao. Bila kupoteza muda aliingia chumbani kwa mama yake. Alimkuta mama yake akiwa amekaa kitandani na kichwa kakiinamisha chini. Shida alimsogelea na kukaa karibu yake kisha akauliza,
“Unajiskiaje mama?”
“Nahisi kuchoka mwili mzima mwanangu vipi umefanikiwa?”
“Ndio mama. Hii hapa…” alipapasa ile khanga akitaka afungue lile fundo amshangaze mama yake kwa kiasi cha fedha alizopata sokoni. Mara uso wake ukabadika ghafla baada ya kuona kuwa ile khanga imekatwa na pesa haimo.
“Mungu wangu! Nimeibiwa mie mama!” Shida aliweweseka huku akirandaranda huku na kule akiwa haamini macho yake.