Shamba la Dhahabu
Mtoto Swala alijitupa katikati ya vijituta viwili vinavyoitunza miili ya wazazi wake ambao walikuwa tayari wamekwisha jilalia. Alikuwa na majonzi na huzuni kubwa kuyaaga makaburi hayo. Hakujua kama angerejea tena kuyaona, maana tayari mkuu wa ukoo wao, mzee Tembo, alishatoa amri ya kumtoa roho kama asubuhi ingemkuta kwenye kiwanja kile cha urithi. Aliweka vibuyu viwili kwenya makaburi yale akawaomba mizimu ya wazazi wake imuongoze huko aendako. Kisha alirejea kibandani, akachukua mihogo miwili na kibuyu cha maji tayari kwa safari.
Njiani, mtoto Swala alitembea kwa hofu kubwa. Alihisi kuwa hata vivuli vya miti vilivyoletwa na mbalamwezi vilikuwa vikimfuata. Sauti za mbweha wenye njaa jioni hiyo zilimtia woga usio kifani. Alikiona wazi kifo kikimnyemelea. Alijua muda si muda atakuwa kitoweo. Kila alipopiga hatua mbili tatu alisimama na kuangaza macho yake pande zote. Baada ya kutembea kwa muda mrefu, mtoto Swala aliona ni heri apumzike kichakani, mahali ambapo wanyama wakali wasingemuona kirahisi. Aliwaomba tena mizimu ya wazazi wake kisha akajilaza.
Alitembea kwa siku tatu bila kuona hatma ya safari yake. Alirandarada huku na huko akitafuta mahali salama atakapoishi. Alinyeshewa na mvua za masika zilizoambatana na upepo na baridi kali iliyopenya hadi kwenye mifupa. Usiku roho yake ilikua juu juu, asiweze kupata hata lepe la usingizi. Akili yake ilivuta taswira ya kifo cha wazazi wake. Alikumbuka usiku ule wanaharamu wale wawili na mzee Tembo walipokuja nyumbani na visu. Alimuona mama yake akigaragara chini na kulia kwa uchungu kisu kikali kilipotoboa tumbo lake. Alimuona baba yake aking’olewa pembe zake na kukatwa kichwa.
“Sikubali, sikubali kabisa! Lazima akione cha mtema kuni!” Mtoto swala alijisemea huku akilia kwa kwikwi. Njaa nayo ilimfanya achoke zaidi. Usiku wa watatu, mtoto Swala alikuwa amekata tamaa kabisa. Aliona hakuna faida ya kuishi kwenye dunia iliyo tayari kummeza. Alisonga mbele hatua tatu kuelekea kwenye mbuyu akaketi chini. Kisha akachukua kijiti kilichochongoka pembeni na kukielekeza kwenye tumbo lake.
“Eeenhhh! Mama yangu eeenhh! Mizimu ya baba yangu nipokeeni huko nakuja.” mtoto Swala alifanya sala ya mwisho kisha aakanza kutoboa tumbo lake.
“Hapana!”
“Niacheni! niacheni tafadhali!”
“Niacheni nikamwone mama’angu.”
Ni sauti iliyoishia na mwangwi. Mtoto Swala alishtuka akasitisha kwanza shughuli ya kujiua. Alikishusha chini kijiti kile huku akitetemeka. Aliona mwanga mkali mbele yake. Alipogeuka aliishia kupata ganzi alipomuona Mama yake akiwa ameketi kwenye gogo. Pembeni kulikuwa na kibuyu na mkuki. Alikuwa akibubujika damu mdomoni na machoni. Mtoto swala alianguka chini puu! fahamu zishamtoka.
“Amka mwanangu amka!”
“Mimi mama yako nitakusaidia.”
“Utachukua kibuyu hiki, kisha utakifungulia shambani, kisha utapanda kilichomo. Utavuna dhahabu mwanangu, tafadhali usiache mkuki huu utakulinda. Mwanangu, kamwe mkuki huu usiue hata mmoja wa ndugu zako.” Sauti iliishia nakutokomea mitini.
Mtoto Swala aliamka asubuhi akachukua kibuyu na mkuki tayari kwa safari. Safari ya siku hiyo ilikuwa ni ya baraka tele. Alitembea kwa muda kidogo, kisha kwa mbali akaona vibanda. Alifurahi maana alijua ameachana na msitu. Alipofika kijijini humo familia moja ilimpatia kiwanja na kibanda kidogo cha kuishi. Mtoto Swala alifurahi sana. Moyo wake ulikuwa uko juu ya dhahabu tu.
“Nani kama Mama jamani! Kanitoa tumboni kanilea na leo kanipa dhahabu hakika mama ni mama hata kama yuko kaburini.” mtoto Swala alijisemea.
Siku ya kwenda kupanda dhahabu mtoto Swala alikuwa na shauku ya kufungua kibuyu ili kuona nini kilichomo.
“Hivi kweli ni mbegu hizi?” alitikisatikisa kibuyu kile ili kusikia nini kilichomo. Alipofika shambani alikifungua harakaharaka. “Loooh! kumbe mpunga? Heee! Kweli hakuna lisilowezekana kwa mzimu wa mama.” Alipanda mbegu zile kwa bidii kwa kuwa alijua muda mfupi zitakuwa dhahabu.
Siku nne zilipita. Baada ya mvua kunyesha mtoto Swala alirejea shambani. Kichwani kwake aliona picha ya shamba lile la dhahabu. Alipofika shambani alitahamaki kuona mpunga umeshamiri katika shamba lile. Alichoma mkuki wake ardhini.
“Hee ni dhahabu gani hii? Au mama alinidanganya tu? Au ukikomaa ndio utageuka dhahabu?” mtoto Swala alijiuliza maswali hayo huku macho yake yakiwatazama ndege waliokuwa wanafaidi mpunga ule.