Sauti Yangu

Art Type: Short story
Artist Name: Safi George

Siku moja, Baba Suzana alipata mkopo (mkadi) na kumpa dada yake ili aongeze maarifa na kuendeleza kazi yake. Hata hivyo, hali ya familia yake haikuwa ya kupendeza. Maisha yalikuwa magumu, chakula kilikuwa ghali, na kipato kilikuwa kidogo. Mara nyingi Mama Suzana alitamani kuomba msaada, akisema moyoni, “Baba Suzi tukumbuke na sisi, ili nasi tuishi kama watu wengine na kulea kwa mapenzi.”

Ili kusaidia familia, Mama Suzana aliamka mapema na kuanza safari ya kuuza chakula mjini na vijijini. Alifanya kazi kwa bidii kubwa na kwa juhudi zote ili mtoto wake asipate njaa. Ingawa alikuwa na furaha ya kuwa na familia yake, moyo wake ulikuwa umejaa wasiwasi. Siku moja mtoto wao alianza kulia kwa njaa. Mama Suzana alihuzunika na kusema, “Sasa tutakula nini, na mtoto analia?” Kwa hasira na msongo wa mawazo, Baba Suzana alimpiga mke wake kibao. Kitendo hicho kilimuumiza sana Mama Suzana, si kwa maumivu ya mwili tu, bali hata moyoni. Aliondoka kwa huzuni na kwenda kwa jirani, akilalamika juu ya mateso yake na hali ngumu ya maisha. Baadaye, Mama Suzana alirudi nyumbani na kumkuta mtoto wake amelala. Alimlisha chakula kidogo alichopata na kumtuliza. Muda mfupi baadaye, Baba Suzana alirudi nyumbani. Alimkuta mke wake kimya, akamsogelea, akambusu na kumkumbatia kwa upendo. Mama Suzana, akiwa na maswali moyoni, alimuuliza: “Je, kwa nini ulinipiga? Nimefanya kosa gani?” Baba Suzana alijibu kwa sauti ya majuto: “Samahani sana mke wangu, usiniache. Nakupenda sana. Nimekosea.”

Walikaa pamoja, wakala chakula chao kwa utulivu na kuanza kupanga mipango ya familia yao. Hata hivyo, hali ya maisha iliendelea kuwa ngumu. Mama Suzana alienda kulima mboga kwa siri ili kuongeza chakula nyumbani. Alifanya kila alichoweza kuhakikisha mtoto wao anapata chakula. Lakini bado mtoto aliendelea kulia kwa njaa mara kwa mara. Kwa huzuni Mama Suzana alisema, “Mume wangu, kwa nini unanifanyia hivi? Mbona hutaki kuhudumia familia?” Baba Suzana alimwangalia kwa upole na kusema, “Samahani sana. Nimekuwa na shida ya kupata chakula. Nimefanya makosa, lakini nitabadilika. Nitafanya mambo mazuri kwa ajili ya familia yetu.” Ingawa kulikuwa na migogoro, walijaribu kupatana na kuendelea kupambana na hali ya maisha. Mama Suzana aliendelea kuwa na uvumilivu, akibeba mzigo wa familia kwa upendo na matumaini.

Gallery

Share the Post: