Msichana Initiative ni shirika lisilo la kiserikali lililoanzishwa mwaka 2016. Linajihusisha na maswala ya kupigania haki ya elimu kwa mtoto wa kike.
Shirika hili linasimamia na kuhakikisha usawa wa kielimu unapatikana kwa wote bila ubaguzi wa aina yoyote, kama vile kijinsia, hususan kwa mtoto wa kike. Pia linasimamia upatikanaji wa fursa za kielimu, kuimarisha ulinzi wa mtoto na kuhakikisha vifaa vya hedhi vinapatikana kwa gharama nafuu pamoja na kuhakikisha mabadiliko ya sera zinazohusu ustawi wa mtoto wa kike zinaendana na uhalisia wa kumuinua mtoto wa kike.
Lengo kubwa la shirika hili ni kuhakikisha jamii ya kitanzania inatambua na kusimamia na kutambulika kwa haki za mtoto wa kike, kuthaminiwa utu wake na kupata nafasi ya kuonyesha na kukuza vipaji vyao bila wasiwasi.
Shirika hili pia lina dira ya kuondoa dhana yoyote ya kibaguzi kwenye mifumo ya kisheria hasa kwa watoto wa kike na kuhakikisha wanahusika kwenye mambo ya kijamii.
Misingi ya shirika hili ni uadilifu na kuzingatia misingi ya kitaaluma kwenye utendaji wake na kuhakikisha linasimama kua mfano hai wa kazi zake kwa jamii.
Uwajibikaji wenye kuleta tija na mabadiliko katika jamii ni sehemu ya nguzo msingi kwa Msichana Initiative. Ushirikishwaji wa makundi mbalimbali ya kijamii na kutoa fursa na huduma kwa watu wote bila kujali jinsia, rangi, umri na hali ya kiuchumi.
Shirika hili linaamini kwenye misingi ya kufanya kazi pamoja na wadau wengine wa maendeleo ikiwemo Serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali na watu binafsi wenye lengo la kufanikisha malengo ya shirika hili.
Sara Beda ni Afisa Mawasiliano wa Msichana Initiative. Anasema shirika lao linafanya kazi na jamii kwa ujumla na kwa upande wa wasichana wanaoshugulika nao ni hasa wale wa shule za msingi na sekondari.
“Kwa upande wa Serikali tunashirikiana na madawati ya jinsia ambayo yanafanya kazi kwa karibu sana na wanajamii ambao wako mstari wa mbele kabisa kuhakikisha wanatoa taarifa pale unyanyasaji unapotokea au kama kuna taarifa za mtoto wa kike kuingizwa kwenye ndoa za utotoni.
Jitihada kipindi cha Covid-19
Mara baada ya mlipuko wa Covid-19 wanafunzi walipitia wakati mgumu kimasomo. Lakini jitihadi zilichukuliwa kuhakikisha wanafunzi wanaendelea kupata elimu.
Kuna club nyingi ziko mashuleni ambazo huwa na lengo la kuwasaidia wanafunzi kua na uelewa wa mambo mbalimbali. Msichana Amani Club ni moja ya kilabu ambazo ziko mashuleni zinazokutanisha watoto wa kike na wa kiume wote kwa pamoja kwa lengo la kujadili mambo mbalimbali ya kimaisha na kimasomo pia hususan mambo na changamoto wanazokutana nazo shuleni na nyumbani.
Pia kuna majukwaa mbalimbali kama jukwaa la ajenda ya msichana. Jukwaa hili hukutanisha wasichana mara moja kwa mwaka kutoka vyuoni, shuleni na mitaani kwa lengo la kujadili mambo yanayomuhusu msichana na nini kifanyike
Kupitia jukwaa la ajenda ya msichana kwa kushirikiana na Serikali Msichana Initiative ilifanikiwa kujadili kwa pamoja mambo ya msingi msichana anatakiwa kuzingatia anapokutana na ukatili wa kijinsia akiwa nyumbani, shuleni au eneo lolote.
Wakati wa Covid-19 mwaka jana kwenye kipindi ambacho watoto walikua nyumbani Msichana Initiative waliandaa kampeni inayoitwa Corona isiwe kikwazo na walitumia mitandao ya kijamii kuhakikisha inafikia watu wengi maana wakati huo matumizi ya mitandao ya kijamii yalikua kwa asilimia kubwa.
Hii ililenga kuikumbusha jamii kua Corona isiwe kikwazo kwa watoto wa kike walio nyumbani kunyanyaswa, kupewa mimba na kutopata huduma zingine za msingi za kijamii.
Wakati wa Covid-19 pia shirika lilinunua barakoa 1000 na kuwagawia wanawake wanaofanya biashara kwenye soko la Kivukoni. Waliona umuhimu wa kugawa barakoa hizo kama sehemu ya kumsaidia mwanamke anayehangaika kuleta chakula nyumbani bila kujali hali ya maambukizi yalikua makubwa kwa kiasi gani.
Na wakati huo huo tarehe 28 mwezi May ni siku ya hedhi salama duniani. Waliona ni vema kuanzisha kampeni iitwayo ‘Vunja Ukimya Corona Isiwe Kikwazo’ kwa lengo la kuwakumbusha wanajamii kuongea na watoto wao wakiwa majumbani na kuhakikisha wanawapa mahitaji husika yanayohitajika bila kujali kuwepo kwa ugonjwa wa Corona