Profile Photo

WAJIKI – TAASISI YA WANAWAKE KATIKA JITIHADA ZA MAENDELEO

  • Public Group
  • 9 months, 3 weeks ago
  • 1

    Posts

  • 1

    Members

Description

Wajiki ilivyoanzishwa
Taasisi ya Wanawake katika Jitihada za kimaendeleo – Wajiki, yenye makao yake makuu Kinondoni Jijini Dar es Salaam ilianzishwa kutokana na shahuku ya Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Janet Mawinza, ya kupigania haki za wanawake ambapo mwaka 2007 alianzisha vikundi vya ujasiriamali. Mawinza ni mwanamke mwenye kiu ya kuona wanawake wakiishi bila kunyanyaswa, huku pia wakifanikiwa kiuchumi.
“Harakati za kujifua kwa ajili ya harakati za wanawake zilianza mwaka 2007. Siku moja niliona tangazo kwenye runinga ikitoa wito wa mkutano wa wanawake uliofanyika Mabibo. Nilimshawishi rafiki yangu, tukahudhuria mkutano ule na kujifunza kuhusu haki za wanawake. Mwaka 2009 tulianzisha vikundi vya Vicoba kwa lengo la kuwawezesha wanawake kiuchumi. Baada ya hapo tukaanzisha kampeni za kupinga ukatili kwa wanawake,” anasema Mawinza, akiongeza kuwa licha ya kuanzisha harakati hizo zote, kikundi chao hakikusajiliwa hadi ilipofika mwaka 2014
“Tumekuwa tukifanya kazi tangu mwakia 2009 lakini tulisajiliwa mwaka 2014. Tumekuwa tukiibua vitendo vya ukatili tukishirikiana na jamii. Tulianzisha kampeni ya ‘Mlango kwa Mlango’ ambayo inatusaidai kufanya kazi zetu, ambapo tunashirkiana na Polisi au hospitali na hata mahakamani na vituo vya msaada wa sheria.
Ili kufanikisha kazi za taasisi walilazimika kujiunga na mitandao mbalimbali ukiwemo Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Mtandao wa Mapambano ya Rushwa ya Ngono, wakaingia pia kwenye Mtandao wa Wanawake, Katiba na Uchaguzi.
Kutokana na uchapakazi wao, hatimaye, Wajiki ilianza kupata misaada na hatimate Kituo cha Msaada wa wanawake Kisheria (WLAC) kilijitokeza na kuwafadhili katika mapambano ya utetezi wa wanawake, huku taasisi ya Women Fund nayo ikiwafadhili kupitia mtandao wa Wanawake Katiba na Uchaguzi kwa lengo la kuelimisha jamii kuhusu mapambano ya rushwa ya ngono.
“Kupitia ufadhili huo tumeanzisha kampeni ya ‘Safari salama bila rushwa ya ngono kwa wasichana na wanafunzi inawezekana’,” anasema.
Akifafanua zaidi kuhusu kampeni hiyo sasa inayotimiza miaka mitatu, Mawinza anasema waliona tatizo la wasichana kupewa mimba limekithiri hivyo walitafuta wadau wanaohusika ili kupiga kampeni ya kupambana nalo.
“Tulianzisha klabu za wanafunzi ambapo wanafunzi walieleza changamoto wanazozipata wanapokuwa katika safari ya kutoka nyumbani kwenda shule na kurudi. Baada ya kuona changamoto hiyo tukawashirikisha madereva wa bodaboda na daladala na kujadiliana jinsi ya kuwasaidia wanafunzi wa kike. Kwa hiyo tukaanzisha vikundi vya madereva wa bodaboda tukawa tunawafuata kituo kwa kituo,” anasema.
Wajiki waliutekeleza mradi huo katika kata ya Makumbusho, Manispaa ya Kinondoni katika shule tano za msingi na Sekondari moja na kwa manispaa ya Ilala walifanyia katika kata ya Gongo la Mboto kwa kukutana na baadhi ya wanafunzi.
Kupitia kampeni hiyo walitumia viakisi mwanga (reflector), vipeperushi na nyimbo, huku pia wakiibua vinara wa mapanmbano hayo mitaani ili kuhamasisha jamii ili ielewe rushwa ya ngono ni ipi.
Kutokana na harakati zake za ukombozi wa wanawake, taasisi ya Wajiki imejulikana na kufanya kazi za taasisi za kimataifa zikiwemo za Umoja wa Mataifa za UN Women (Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake na UNFPA (Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu).

Wajiki ilivyopambana kuwatetea wanawake wakati wa Corona
Mwaka 2020 haukuwa salama katika kila nyanja ukianzia kiuchumi, kijamii na kisiasa, kwani nchi nyingi zilisimamisha shughuli za wazi zinazohusisha mikusanyiko ya watu wengi. Tanzania, kama zilivyo nchi nyingi ilifunga baadhi ya shughuli zenye mikusanyiko ikiwa pamoja na kufunga shule zote na kudhibiti usafiri katika mabasi huku pia tahadhari za usafi zikizingatiwa.
Wanawake ndiyo kundi lililoathiriwa zaidi wakati huo, kwani wengi wao shughuli zao zilitegemea mikusanyiko ikiwa pamoja na ufanyabiashara ndogo ndogo.
Kutokana na changamoto hiyo Wajiki iliamua kutafuta suluhisho.
Mkurugenzi wa Wajiki, Janet Mawinza ameeleza jinsi taasisi yake ilivyopambana kuwasaidia wanawake wajasiriamali kuendelea na biashara zao.
Anasema walishirikiana na taasisi ya Soma kuamzisha mradi wa Mshikamano Hub ambao ulisaidia wanawake wakati wa majanga hasa Corona.
“Wanawake waliathirika zaidi kwa sababu walikuwa wakipanga biashara zao wateja hawakwenda; kwa mfano mwanamke muuza ndizi wateja waliogopa kununua bidhaa kwamba anaweza kuwaambukiza Corona. Kwa hiyo tulitafuta njia ya kutoa sauti na hapo wenzetu Soma waliiona na kuanzisha mradi ambapo sasa mteja halazimiki kwenda kwa mwanamke anayefanya biashara pale. Tuliwatumia madereva wa bodaboda kufikisha bidhaa kwa wateja wao,” anasema.
Hawakuishia hapo, kwani pia walianzisha mradi wa kutengeneza pilipili na karanga ili kuwasaidia wanawake kujipatia kipato wakati wa Corona huku wakipinga ukatili.
“Tukaanzisha mradi wa kutengeneza pilipili, lakini kwenye kifungashio tunaweka karatasi yenye ujumbe wa kampeni yetu. Pia tulitengeneza karanga zenye ujumbe huo,” anasema.
Pia anasema mradi huo uliwawezesha wanawake kutoa taarifa ya matukio ya ukatili kwani katika kipindi cha kufungiwa kutokana na ugonjwa wa Corona baadhi ya wanawake waliofanyiwa vitendo vya ukatili hawakuweza kutoka kwenda kutoa taarifa kwa kuhofia maambukizi.
Kwa upande mwingine, Mawinza anasema waliendelea kutoa elimu ya kupinga ukatili wa wanawake katika kipindi cha Corona kwa kuweka maturubali na vitakasa mikono na kuweka mabango yenye ujumbe wa kupinga ukatili huo.

Groups

Members

Most Liked

Comments

    Featured