Lazima Nifanikiwe
Cecilia Mgimbila
Helena aliketi pembeni kidogo mwa nyumba yao, akiwa chini ya kivuli cha mti mkubwa karibu na jiwe kubwa lililobeba kumbukumbu ya tukio la kusikitisha lililotokea miezi michache iliyopita na kusababisha kifo cha baba yake mpendwa. Akiwa analitafakari tukio lile, alijiuliza kwa sauti, ‘Kwa nini nyoka yule alimgonga baba yangu lakini?’ Alihisi kuna mchezo uliochezwa nyuma ya pazia. Helena alitamani angekuwepo pale wakati baba yake aliposhambuliwa na nyoka. Labda angebaini kitu. Kifo cha baba yake kilikuwa kimeondoa furaha ndani ya familia yao. ‘Laiti baba angalikuwa hai, angeyashughulikia yote yanayotusibu.’ Helena aliendelea kuwaza kwa majonzi.
Kwa mbali alikuwa akimtazama mama yake, ambaye alikuwa na tumbo kubwa lenye kiumbe kinachokua ndani yake. Mama alikuwa ameketi kwenye mkeka akiwa kaegemea mikono yake na kuvuta pumzi kwa kasi. Helena alijaribu kulinganisha majukumu makubwa yaliyokuwa mbele yake na umri wake wa miaka kumi na sita. Alikumbuka jinsi baba yake alivyokuwa mwepesi wa kushughulikia kila jambo gumu lilipotokea. Lakini sasa, majukumu yote yalimwangukia yeye na mama yake.
”Helena, Helena!” sauti ya Mama ilimtoa Helena katika lindi la mawazo.
“Helena!” Mama aliita tena.
“Naam!” Helena aliitika huku akishuka juu ya jiwe na kuelekea alikokuwa ameketi mama yake.
“Helena inabidi umkamate kuku mmoja ukamuuze.” aliongea Mama huku akiwa ameipakata mikono yake na kumtazama mwanae usoni.
“Kuku tena! Ndio mali pekee tuliyobakiwa nayo, mama.”
“Ukichelewa tutampoteza,”mama yake alimjibu kisha akatema mate chini.
“Tutampoteza nani?”aliuliza Helena.
Mama Helena mkazia macho yake huku akilipapasa tumbo lake. Hali ile ilimuonyesha Helena yakuwa Mama yake hakuhitaji mzaha mzaha wakati ule.
“Sawa mama.” Helena alijibu kinyonge kuondoka kuelekea nyuma ya nyumba yao kutekeleza agizo la mama yake. Alikuta kuku watatu wakidonodonoa na kuparuaparua ardhini. Aliwatazama kwa makini ili kujua yupi angeuzika kwa urahisi. Aliamua kumkimbiza jogoo mmoja aliyenona. Jogoo alikimbia lakini akanasa kwenye miiba. Helena alimrukia kama paka shume lakini jogoo alifurukuta akawahi kutoka na kumuacha Helena akiwa amejikwaa na kuangukia kwenye miiba.
“Aaaah asiii…!” aliguna Helena wakati anajizoazoa. Alinyanyuka na kuchomoa miiba iliyokuwa mwilini mwake. Alikuwa amevaa shati la mikono mifupi na kaptula. Aliendelea kumkimbiza jogoo ambaye alikwishaingia kwenye vichaka vikavu vilivyoparua mwili wake.
“Nikikushika nitakufundisha adabu,” Helena alijisemea akiwa amekunja ndita. Jogoo alikimbia na kuingia jikoni akajificha kwenye rundo la kuni zilizokuwa karibu na jiko la mafiga matatu. Helena alimfuata huko huko jikoni, akafunga mlango wa bati lenye kutu akaanza kuzipangua zile kuni. Jogoo aliruka lakini Helena alimwahi akamrukia na kumkamata mguu. Jogoo alipigapiga mbawa zake lakini Helena alimbana kwapani akamfunga mguu yote miwili kwa kamba.
Sauti yenye maumivu makali ilimvamia Helena masikioni mwake, ikamshitua kutoka katikati harakati za kukamatana na kuku. Alimweka chini kuku na kukimbia nje alipokuwa mama yake. Alimkuta mama yake akiwa ameegemea ukuta, akiwa anapumua kwa shida, mkono mmoja ukishikilia tumbo lake na mwingine unakipapasa kiuno chake. Helena aliita kwa hofu, “Mama, mama?”
“Ti…Helena!?” mama yake alikuwa anagugumia kwa maumivu makali.
“Hah! hah! hah! mama, mama?” Helena aliendelea kumwita mama yake huku akihema kwa hofu.
“Mh! Helena…!!!, Kaombe-e…” Mama Helena alijaribu kutoa maelekeza lakini yaliishia njiani kwa jinsi alivyokuwa anagugumia kwa maumivu.
“Ni, nikaombe nini?” Machozi yalimtoka Helena, akamkumbatia mama yake na kumhoji apate kujua nini kilimpasa afanye.
“Msa-a-ada mwanangu mmh! Aahah!”
Helena aliutoa taratibu mkono wake mabegani mwa mama yake na kutimua mbio, akashika njia nyembamba iliyosongwa na nyasi ndefu kiasi. Kwa mbali ilionekana nyumba ya msonge iliyoezekwa kwa nyasi. Mzee wa makamo alikuwa ameketi kwenye kigoda mbele ya nyumba hiyo. Chini alikuwa amejifunga msuli na juu amevalia fulana na koti la mikono mirefu; na baraghashia kichwani.
Helena alifika kwenye nyumba ile akihema. Bila hata salaam, Helena alimvuta yule mzee mkono akasema,
“Twendeehhh!”
“Wapi?” alihoji Mzee Jumbe huku akimtazama Helena kwa macho yenye viulizo vingi.
“Mama aaah, mama aaah, nyumbani!” Helena alijibu huku akimvuta. Mzee Jumbe hakuongeza neno. Alimfuata Helena kuelekea kwao. Walifika nyumbani wakamkuta mama Helena jasho linamtoka, anagugumia akiwa ameuma meno. Helena aliingia ndani na kutoa baiskeli.
“Shika vizuri.” Mzee Jumbe alimwambia Helena alipomuona akitoa baiskeli. Helena alikamata usukani wa baiskeli na kulibana tairi la mbele kwa miguu yake.
Mzee Jumbe alimwinua Mama Helena taratibu, akamkongoja na kumpakia kwenye baiskeli.
“Njoo huku umshike.” Mzee Jumbe alisema akiwa ameshika kitako cha baiskeli kwa mkono mmoja na mwingine akiwa amemshika mama Helena. Helena aliutoa mguu wake taratibu kwenye tairi na kuachia usukani huku akiwa ameshika koti alilokuwa amevaa Mzee Jumbe. Alirudi nyuma taratibu akamwachia Mzee Jumbe ashike usukani na kuikokota baiskeli kuelekea zahanati.
Walipofika zahanati, Mzee Jumbe alimwagiza Helena aende mapokezi akamwite nesi. Helena alitimua mbio akaingia ndani akasimama mkabala na mlango wenye kibao kilichoandikwa MAPOKEZI. Alimkuta muuguzi aliyevalia gauni fupi la kijani aliyekuwa anafunuafunua karatasi zilizokuwa juu ya meza.
“Dada! Dada! kuna mgonjwa nje kazidiwa.”Helena alisema kwa sauti ya juu huku akitweta kwa taharuki.
“Punguza sauti kuna wagonjwa wengine wenye maumivu humu.” alisema yule dada akiendelea kufungua karatasi. Helena aliangaza macho huku na kule lakini hakuona mgonjwa mwingine zaidi ya mama yake. Taratibu nesi alisimama akafungua mlango na kutoka nje.
“Yuko wapi huyo mgonjwa mwenyewe?” aliuliza yule nesi akiwa ameshika kiuno.
“Yupo huku.” Helena alijibu akiwa amenyoosha kidole kuelekea alipokuwepo mama yake. Yule nesi akamfuata nyuma hadi mahali alipokuwepo mama Helena na mzee Jumbe.
“Pole kwa safari baba.” alisema yule nesi na kusogea moja kwa moja hadi alipokuwa Mama Helena. Alikuwa ameegemea ukuta na ameshika kiuno kwa mkono mmoja mwingine ukiwa unalisuguasugua tumbo lake.
“Asante mama.” alijibu Mzee Jumbe.
“Njoo tusaidiane kumuingiza ndani.” aliongea nesi akiwa anajaribu kumkongoja Mama Helena. Mzee Jumbe alisaidiana naye wakaenda hadi kwenye mlango wenye kibao kilichoandikwa WAZAZI. Waliingia ndani Helena akifuata nyuma. Ndani ya chumba kulikuwa na chumba kingine kilichoandikwa LEBA. Ndani kulikuwa na kitanda cha chuma na godoro lililokuwa limetandikwa shuka jeupe. Walimkalisha Mama Helena kitandani kisha nesi akasema, “Mzee unaweza kwenda nje.”
“Sawa mama.” alisema Mzee Jumbe akatoka nje.
“Na wewe unasubiri nini? Nenda nje.” nesi alimwambia Helena.
Helena aliinamisha kichwa chini na kutoka nje. Alimkuta Mzee Jumbe akiwa amekaa juu ya jiwe lililokuwa chini ya mti nje ya zahanati,
“Helena njoo.” Mzee Jumbe alimwita kwa sauti na kwa ishara ya mkono. Helena alisogea taratibu akiwa ameinamisha kichwa chini. Mzee Jumbe alimshika mkono na kumvuta aketi karibu naye.
“Mama atakuwa salama usiwaze. Halafu wewe ni msichana mkubwa sasa, jikaze.” Mzee Jumbe alimfariji Helena huku akimpapasa mgongoni na kumuaga. Helena alitikisa kichwa, akafuta machozi yaliyokuwa yakimbubujika. Mzee Jumbe alipanda baiskeli na kuondoka huku Helena akiwa kimya, anamtazama.
Helena akiendelea kusubiri. Nusu saa baadaye alimwona nesi akitoka akiwa anatoa mipira aliyokuwa amevaa mikononi na kuitupa ndani ya ndoo ya taka. Helena alinyanyuka na kumfuata nesi ili aulizie hali ya mama yake. Nesi aliingia moja kwa moja hadi kwenye chumba cha mapokezi. Helena alimfuata na kumuuliza,”Naruhusiwa kumuona?”
“Bado. Kwanza kamwite baba yako.” alijibu yule nesi kwa mkato.
Kwa unyonge Helena akajibu, “Hayupo.”
“Kaenda wapi?”
“Alishafariki.”
“Na yule uliyekuja nae ni nani?”
“Ni jirani yetu.”
“Hee makubwa! Sasa pesa anatoa nani?” Nesi alihoji akiwa ameshika kiuno.
“Hela ya nini?”
“We mtoto, sihitaji maswali.” Alisema yule nesi akimnyooshea kidole Helena ambaye alikuwa anamkodolea macho tu pasipo kuwa na jibu la kumpa.
“Kimbia kawaambie ndugu zako inahitajika elfu sitini sasa hivi.”
“Ya nini?” alihoji Helena kwani hakujua kiasi kikubwa hivyo cha pesa ni cha nini na angekipata vipi.
“Sihitaji maswali fanya nilichokwambia,” alifoka yule nesi.
“Asa wakiniuliza ya nini niwaambiaje?” Helena aliendelea kuhoji akiwa amemkodolea macho nesi yule,
“Nenda kawaambie ndugu zako inahitajika hela kwa ajili ya vifaa vya kujifungulia mama na hela ya kitanda kwa sababu atatakiwa kukaa hapa kwa muda baada ya kujifungua, haya nenda upesi.”
“Lakini…!!!”
“Lakini nini?” nesi alimkata kauli.
“Akina mama wajawazito na wazee wanapatiwa huduma bure.” Helena alikomaa.
“Nani kakwambia? Nenda kachukue hela acha kufanya mzaha.”
“Mimi nilisikia redioni.”
“Ukiendelea kufanya ubishi utampoteza mama yako bure. Fanya hima, hakuna muda wa kupoteza.” Helena alilia aliposikia maneno ya kifo. Alipiga magoti na kushika pindo ya gauni la nesi.
“Nakuomba umsaidie mama yangu nesi mimi sina hela.”
“We hebu niache!” alisema nesi huku akivuta gauni lake lililokuwa limeng’ang’ania mikononi mwa Helena.
“Lakini mama yangu anapaswa kutibiwa bure.”
Nesi alimtazama Helena na kubetua midomo yake.
“Mama yangu lazima atibiwe haiwezekani.” Helena aliendelea kulalama.
“Sipendi kubishana na watoto. Toka ukapigie kelele zako huko nje.” Nesi alisema akaanza kumsukuma Helena atoke nje. Helena alipepesuka lakini hakuondoka. Huku machozi yakiendelea kumtoka aliendelea kumuelimisha nesi yule,
“Wajawazito wanatakiwa kutibiwa bure, usitoe wala kudai fedha, Hivyo ndivyo nilivyosikia redioni.” Hakutaka kumpa nafasi nyingine ya kuzungumza. “Sasa nitatembea kwa mguu hadi ikulu nikaulize kama taarifa hizi ni za uongo. Mama yangu akifa mikononi mwako, ujue na wewe huna maisha . . .”
“Fumba mdomo wako,” nesi alifoka, lakini akionekana kutishika. “Usiniletee uchuro mimi. Mama yako atatibiwa, kaa kitako hapo chini usubiri.”
Nesi alimtazama Helena na kuingia kwenye chumba kimojawapo. Hatimaye aliibuka na kisahani chenye vifaa vya kujifungulia. Aliingia nacho chumba cha kujifungulia. Muda si mrefu sauti ya kichanga ilisikika kutoka kwenye kile chumba alichoingizwa Mama Helena. Helena akasimama kwa mshtuko huku akitazama mbingu, na uso wake ukavaa tabasamu.